Kufuatia tukio la kutitia kwa choo cha wanafunzi, shule ya Msingi Seliani, halmashauri ya Arusha wilayani Arumepru, Kampuni ya Eco Valley Advisers inayojihusisha na kampeni ya Nyumba ni Choo, imetimiza ahadi yake kwa kutoa, msaada wa masinki 21 ya vyoo, yenye thamani ya shilling 253,000, kwa lengo kuchangia ujenzi wa choo kipya, mara baada ya kutitia kwa choo hicho.
Akikabidhi masinki hayo, kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Arusha, Meneja wa kampuni hiyo Avit Buchwa, amesema kuwa, wametoa masinki hayo baada ya kupata taarifa za kutitia kwa choo cha wanafunzi, kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo, Mheshimiwa Jerry Muro, wakaona ni vema kutoa msaada huo ili wanafunzi hao wapate mahali salama pa kujisaidia kwa haraka bila kuathiri ratiba yao ya masomo.
Meneja Buchwa, ametoa ufafanuzi juu ya masinki hayo kuwa, sinki 1 kati ya masinki 21 waliyoyatoa ni maalumu kwaajili ya wanafunzi walemavu, huku masinki 20 yakiwa kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi wasio walemavu na kuongeza kuwa, masinki hayo yametengenezwa kwa malighafi ya plastiki ambayo ni rahisi kwa matumizi kwa watoto wa rika zote hivyo yataongeza usalama wa watoto pindi watakapokuwa wakitumia.
"Haya masinki yana kifuniko maalumu kinachotenganisha shimo na sehemu ya juu, hivyo ni salama kutumiwa hata na mtoto mdogo bila kuhofia kutumbukia, pia mfuniko huo unazuia harufu mbaya ya choo kutoka nje na pia kuzuia wadudu kama inzi na mende kuingia au kutoka chooni, hivyo ni salama zaidi kwa afya" amethibitisha Buchwa.
Pia ameongeza kampuni ya Eco Valley Advisers imeamua kutoa masinki hayo, ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu ya Elimu na kuwafanya watoto wa kitanzania kusoma katika mazingira salama na rafiki.
Hata hivyo ameishauri jamii kutumia masinki hayo kwaajili ya usalama wa afya zao, na kuwa gharama zake ni za chini kwa mwananchi wa hali ya chini kumudu kununua, ukilinganisha na gharama kubwa za masinki za malumalu na pia matumizi yake ni rahisi hata kwebye maeneo yenye shida ya maji kwani hutumia maji kidogo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwapatia masinki hayo, ambayo yatawezesha ukamilishaji wa ujenzi wa choo hicho mapema na wanafunzi kuanza kukitumia huku akiwataka wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya Elimu.
Aidha amewaahidi kukuanza kutumia aina ya masinki, katika ujenzi wa vyoo vya shule hasa kwenye maeneo yanye shida ya maji na kwa kuwa ni rahisi kutumika kwa rika zote na zaidi yatasaidia kuwa na uhakika wa usalama wa mtoto pindi anapoyatumia.
Afisa mtendaji wa kata ya Kimnyaki, Joshua Jonas licha ya kuishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo, amethibitisha kuwa, tayari ujenzi wa choo hicho umeshaanza, na uko katika hatua za awali ya msingi, msingi ambao umechimbwa na wananchi wenyewe wa Kimnyaki.
Msaada huo wa masinki ya vyoo ni miongoni mwa ahadi za michango ya wadau mbalimbali, kufuatia tukio la kutitia kwa choo cha wanafunzi wa shule ya msingi Seliani, tukio lililotokea mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.