Na.Elinipa Lupembe.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo, kufanyakazi kwa weledi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa Umma, wakisimamia kanunini ya uadilifu, uwajibikaji, umakini na upendo huku msingi wao mkuu ukiwa ni kufanya kazi kama timu.
Mkurugenzi Msumi ameyasema hayo wakati wa mkutano wake wa kikazi na watumishi wa Makao Makuu ya halmashauri, mkutano ambao ni wa kimkakati katika kuboresha hali ya uwajibikaji, utendajikazi na utekelezaji wa majuku kwa kila mtumishi kisekta, mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Msumi amewasisitiza watumishi hao, kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kila mmoja kwa nafasi yake na kulingana na taaluma yake aliyoajiriwa nayo, huku kila mtumishi akitambua na kuthamini umuhimu wa mtumishi mwingine kiseta, jambo ambalo wakifanya kazi kama timu, watafikia maono ya halmashauri hiyo kwa wepesi, maono yanayojibainisha kuwa halmashuri inayoongoza kwa kutoa huduma bora kwa jamii kwa maendeleo endelevu.
"Watumishi wenzangu, Serikali imewaamini, imewapa dhamani ya kuwahudumia wananchi itumikieni serikali hii kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake bila kusukumwa, wahudumieni wananchi kwa kuwa ndio jukumu letu kubwa, tufanye kazi kama timu, kila mtumishi hapa anao umuhimu wake katika kufikia malengo ya halmashauri na serikali kwa ujumla, nguzo zetu ziwe ni uadilifu, uwajibikaji, umakini na upendo katika eneo la kazi, ukiwa mwadilifu, utawajibika kwa umakini, ukiwa na upendo utamthamini mwingine na kufanya kazi kama timu na kufika malengo ya halmashauri yetu".
Amesisitiza Mkurugenzi huyo.Aidha amewasisitiza watumishi hao, kuwahi kazini na kila mmoja kuwa na mpango kazi wake utakaomuongoza kutekeleza majukumu yake ya kila siku pamoja na kufanya tathmini ya utekezaji wa mpango kazi huo, huku akiwataka kuhakikisha kila mtumishi anajaza fomu za Opras, fomu ambazo ni dira ya utekelezaji wa mpango kazi na tathmini ya uwajibikaji wa mtumishi kwa kipindi cha nusu mwaka mpaka mwaka mzima.
"Kila siku unapokwenda kazini, hakikisha unafahamu unakwenda kufanya nini kwa kuzingatia mpango kazi wako wa siku, na unapoondoka jioni unajipima utekelezaji wako kwa kutathmini yaliyotekelezeka na kama hayajatekelezeka yawekee mkakati wa utekelezaji wake, kwa kufanya hivyo, halmashauri itafikia malengo yake na serikali kwa ujumla, kwa maendeleo ya taifa letu" ameweka wazi Mkurugenzi Msumi.
Wakati huo huo amewataka wakuu wa Idara na Vitengo kuhakikisha wanafanya vikao vya idara na vitengo vyao kama kanuni zinavyoelekeza, na kutoa nafasi kwa watumishi, kuweka wazi changamoto zao ili zitatuliwe ndani ya idara zao kwa wakati na sio kusubiri kutatuliwa na mkurugenzi, huku wakisimamia maadili ya watumishi pamoja na uwajibikaji kwao kwa kutumia hekima, busara na maarifa yatakawezesha wananchi kupata huduma bora kupitia huduma zinazotolewa katika Idara husika.
Hata hivyo watumishi wa halmasahuri hiyo, wamempongeza mkurugenzi huyo kwa kuweka wazi msingi wa utendaji kazi wake na kuahidi kufanya kazi kwa bidii huku wakimuomba kutatua baadhi ya changamoto zinazokwamisha utendaji kazi na uwajibikaji wa haraka katika maeneo yao ya kazi, ikiwemo vifaa vya kufanyia kazi, mazingira rafiki ya kazi pamoja na usafiri wa kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kuzitatua kero zinazowakabili wananchi kwa wakati.
Kikao kazi hicho ni cha kawaida ambacho huwakutanisha watumishi hao na mkurugenzi mtendaji, kikiwa na lengo la kukumbushana utekelezaji wa majukumu ya kila mtumishi kisekta, na kujenga uelewa wa pamoja wa namna bora ya kufikia malengo ya halmashauri, kwa uzingatia maono na dira ya halmshauri katika kujenga taifa la Tanzania.
Arusha DC
KaziInaendelea✍✍✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.