Na. Elinipa Lupembe.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo, kutekeleza wajibu wao kwa kutambua majukumu yao ya kiutumishi kwa kufanyakazi kwa kujiamini huku wakisimamia maadili ya utumishi wa Umma.
Mkurugenzi Mtambule, amesema hayo alipokutana kwa mara ya kwanza na watumishi wa makao Makuu ya halmashauri hiyo, kwenye kikao chake cha kujitambulisha, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, mara baada ya kuanza kazi rasmi katika halmashauri hiyo, baada ya uteuzi wake uliofanywa na mheshimiwa Rais mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mkurugenzi huyo amewataka watumishi hao, kufanyakazi kwa bidii, huku nguzo kubwa ikiwa ni ukweli na uaminifu katika utendaji wa kazi, kwa kutanguliza utu na uzalendo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi kwa maendeleo ya halmashauri ya Arusha.
Aidha amewataka watumishi hao, kuwa wabunifu katika kazi, ili kazi zao ziwatofautishe na watumishi wa halmashauri nyingine, kwa kuwa majukumu ya utumishi wa Umma yamefanana kwa halmashauri zote, tofauti inakuja katika ubunifu na kuongeza thamani katika utendaji kazi.
"Acheni kufanya kazi kwa mazoe, kuweni watumishi wa tofauti wa kubuni mambo zaidi kwenye kazi zenu, kazi za utumishi wa Umma zinalingana kote, ila ukifanya kitu tofauti kitafikisha halmashauri yetu katika hatua nyingine tofauti" amesisitiza Mkurugenzi Mtambule.
Aidha amewataka watumishi hao kuishi kama familia moja, kwa kupendana, kuelekezana, kubebeana zaidi kufanyakazi kama timu moja kwa kuzingatia miongozo, kanuni na sheria za utumishi wa Umma.
Ameendelea kufafanua kuwa, jukumu kubwa la Watumishi ni kutatua kero za wananchi, hivyo jipeni muda wa kuwasikiliza wananchi, kutumieni lugha nzuri yenye staa, hudumieni wananchi kwa upendo bila kuwabagua, tatueni kero zao kwa kuwambia wananchi ukweli ili kujenga taswira nzuri ya halamashauri yetu.
"Serikali imewaamini na kuwapa jukumu la kuitumikia, tunzeni siri za ofisi na za watumishi wenzenu, hakikisha unafanya kazi kwa nidhamu, kwa kufuata maadili ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwahi kazini na kutumia muda wa kazi kufanyakazi na si vinginevyo" amesema mkurugenzi huyo.
Nao watumishi wa halmashauri hiyo, wameahidi kumpa ushirikiano, mkurugenzi huyo kwa kutekeleza majukumu yao bila kusukumwa, kwa kuzingatia maafili ya utumishi wa Umma, lengo likiwa kutoa huduma bora kwa wananchi wa halmashauri ya Arusha.
Akimkaribisha Mkurugenzi huyo kwa niaba ya watumishi wa halmashauri ya Arusha, Kaimu Afisa Utumishi, Abihud Mwakijambile, amesema kuwa, watumishi hao wako tayari kushirikiana na mkurugenzi huyo mgeni, kufanyakazi kwa bidii kama timu kwa kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa Umma.
"Mkurugenzi karibu sana Arusha DC, watumishi wako tayari kushirikiana nawe, kama ilivyokuwa kwa wakurugenzi waliotanguli, nikuahidi kufanyakazi kwa bidii kama timu ikiwa ni moja ya core value za halmashauri yetu, ambayo iko moyoni kwa watumishi wote"
Mkurugenzi Mtambule ni Mchumi kitaaluma, akiwa ni mkurugenzi wa nne, tangu kuanzishwa kwa halmashauri ya Arusha mwaka 2007, akiwa ameteuliwa na mheshimiwa Rais kutoka Jiji la Mbeya alikotumika kama Afisa Mipango wa Jiji.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.