Na. Elinipa Lupembe.
Jamii imetakiwa kufahamu kuwa ina wajibu wa kuchangia damu na kutambua umuhimu wa kushiriki zoezi hilo ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji hudumu ya damu kwa dharura ikiwemo kina mama wajawazito na watoto licha ya kuwa zoezi hilo ni la hiari.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, alipokuwa akichangia damu, wakati wa zoezi maalum la uchangiaji wa damu salama, lililohusisha watumishi wa halmashauri hiyo na wageni waliofika kupata huduma katika halmashauri hiyo kwa siku hizo za zoezi hilo.
Mkurugenzi Mtambule ameweka wazi kuwa, licha ya kuwa uchangiaji wa damu ni jambo la hiari, lakini kuna umuhimu mkubwa wa kila mtu kutambua wajibu wake wa kuchangia damu, kutokana na uhitaji mkubwa wa damu kwa wagonjwa wa dharura katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
"Kama tujuavyo, uhitaji wa damu ni wa dharura na kila mtu anapaswa kujua kuwa, muda wowote yeye ni muhitaji wa damu kwa dharura, hivyo tuna wajibu wa kujitolea kuchangia damu, ili kuwa na damu ya kutosha katika benki za damu, jambo lililotusukuma kuendesha zoezi la hiari kwa watumishi wa Arusha DC, tukiwa na lengo kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu wakati wote na kuongeza matumaini yao ya kuishi". Amesema Mkurugenzi Mtambule.
Hata hivyo amefafanua kuwa, zoezi hilo limefanyika kutokana na uhaba wa damu kwenye benki ya damu, katika hospitali ya wilaya hiyo ya Olturumet, jambo ambalo lililosababisha kuendesha zoezi la maalumu uchangiaji damu kwa hiari kwa watumishi wa halmashauri ya Arusha, huku watumishi wakijitokeza kushiriki zoezi hilo.
Nao watumishi wa halamshauri ya Arusha, waliojitokeza kuchangia damu katika zoezi hilo, wameupongeza uongozi wa halamshauri hiyo kupitia mkurugenzi mtendaji kwa kuendesha zoezi hilo kwa watumishi ndani ya ofisi zao, zoezi ambalo matokeo yake yanatarajiwa kwenda kuokoa maisha ya wagonjwa hususani mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Afisa Uchaguzi, halmashauri ya Arusha, Hadija Mkumbwa, licha ya kuvutiwa na kushiriki zoezi la uchangiaji damu, amekir kuwa, mara nyingi watumishi wamekuwa ni wahamasishaji wa zoezi la uchangiaji damu, na sio wachangiaji damu, kupitia zoezi hilo maalumu kwa watumishi limewapa fursa ya kuwa ni sehemu ya watu, wanakwenda kuokoa maisha ya watu wengine.
Naye Mganga Mkuu, halmashauri ya Arusha Dkt. Petro Mboya, amewatoa hofu watu wanaoogopa kuchangia damu kuwa, kitendo hicho hakina madhara yotote kiafya kwa mchangiaji damu mwenye afya njema, na kuwataja watu watu wasiofaa kuchangia damu ni pamoja na wenye magonjwa ya kisukari, presha, watu waliofanyiwa upasuaji mkubwa karibuni na wale wanaotumia dawa za muda mfupi na mrefu kwa wakati huo.
Aidha Dkt. Mboya amewashukuru watumishi wote waliojitokeza kuchangia damu, na kukiri zoezi hilo kwenda kwa mafanikio, huku wakiwa wamefanikiwa kukusanya kiasi cha uniti 21 za damu.
Naye Mratibu wa Damu Salama na Afisa Ustawi wa Jamii, halmashauri ya Arusha, Beatrice Tangi, amesema kuwa, zoezi la uchangaji damu ni zoezi la kitaifa ambalo limekuwa likiendelea kila siku, jukumu lao watalamu ni kuhamasisha watu kujitoa kuchangia damu kwani hakuna kiwanda kinachoweza kutengezeza damu ya kumuongezea binadamu, bali ni binadamu pekee ndio wenye uwezo wa kuokoa maisha ya wagonjwa kwa kuchangia damu.
PICHA ZA MATUKIO YA UCHANGIAJI DAMU WATUMISHI WA ARUSHA DC
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.