Na. Elinipa Lupembe.
Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango halmashauri ya Arusha, wameutaka uongozi wa halmashauri hiyo, kuweka vibao kwenye maeneo yote yanayomilikiwa na halmashauri, lengo likiwa kuujulisha umma kwamba maeneo hayo ni mali ya halmashauri ya Arusha, pamoja na kuepusha uvamizi wa maeneo hayo.
Wajumbe hao, wametoa agizo hilo wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya kawaida ya kamati ya Fedha ya kukagua miradi ya maendeleo kwa kila robo ya mwaka, kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha.
Wajumbe hao walikubaliana hayo mara baada ya kutembelea na kukagua maeneo ya wazi yanayomilikiwa na halmashauri, na kukagua eneo lililopo Sekei, Gomba na Mlangarini na kugundua kuwa maeneo hayo yanaweza kupotea kama halmashauri haitachukua hatua za haraka za kuyafanyia matumizi.
Hata hivyo wajumbe hao walikwenda mbali zaidi na kuagiza menejimenti kutengeneza hati miliki za maeneo yote yanayomilikiwa na halmashauri pamoja na kuandaa mara moja mpango mkakati wa matumizi ya maeneo hayo, ili yaweze kutumika kama yalivyokisudiwa kwa manufaa na maendeleo ya wananchi wote.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Ojung'u Salekwa amewasisitiza watalamu wa halmashauri, kuwa ni vema maeneo hayo yakawekwa vibao vya utambuzi vinavyoonesha eneo hilo ni mali ya halamshauri ya Arusha, kuyaandalia hati miliki pamoja na kuandaa mpango mkakati wa kuanza kuyatumia maeneo hayo."Kwa kuanza ni vema kuanza kwa kuweka vibao vya utambuzi, vya kuonesha eneo hili ni mali ya halmashauri ya Arusha, na kuandaa hati miliki pamoja na kuanza kutumia maeneo hayo kwa ajili ya manufaa ya halmashauri na wananchi wote" amesema Mheshimiwa Mwenyekiti.
Kaimu Mkurugenzi, mwalimu Hossein Mghewa licha ya kupokea maagizo na kuahidi kuyaanyia kazi kwa haraka, ameweka wazi umuhimu wa kuhakikisha maeneo hayo yanatambulika kisheria ikiwa ni pamoja na kutengenza hati za hati za maeneo haya sambamba na kuandaa mpango wa matumizi wa maeneo hayo.Aidha miradi iliyotembelewa na Kamati hiyo ya Fedha ni pamoja na eneo la Gomba lenye ukubwa wa mita za mraba 17,948 kwa ajili ya kujenga stendi, eneo la kujenga Soko lenye ukubwa wa mita za mraba 15,517.
Eneo la Mlangarini lililotengwa kwa ajili ya kujenga shule ya watoto lenye ukubwa wa mita za mraba 3, 737, eneo la kujenga uwanja wa michezo lenye mita za mraba 8, 642, pamoja na kujenga majengo ya serikali lenye ukubwa wa mita za mraba 2, 726, na soko mita za mraba 3,404.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.