Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, amefungua mashindano ya michezo shule za msingi - UMITASHUMTA ngazi ya halmashauri, mashindano yenye lengo la kupata timu za kuiwakilisha halmashauri ngazi ya mkoa.
Ufunguzi huo umefanyika kwenye viwanja vya michezo vya shule ya sekodari Ilboru yakishirikisha timu wakilishi kutoka Klasta tano za halmashauri hiyo huku timu za wanafunzi wa elimu maalumu wakipewa kipaumbele cha ushiriki.
Akizungumza wakati akifungua mashindano hayo, Mkurugenzi Mahera, amewataka wanafunzi hao kuwa na nidhamu wakati wote wa michezo na zaidi kuendeleza nidhamu hiyo katika kipindi chote cha masomo yao.
Aidha amewataka walimu wanaosimamia michezo na mashindano hayo, kuhakikisha wanachagua wachezaji wazuri ili kupata timu bora itakayoweza kuleta ushindi kwenye mashindano ngazi ya mkoa huku akipongeza ushiriki wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
" Hakikisheni mnfanya uchaguzi makini na sahihi kwa kuchagua wachezaji wazuri ili kupata timu bora itakayoweza kufanya vizuri kwenye mashindano ya mkoa mpaka taifa" amesema Dkt. Mahera
Akizungumza mbele ya mgeni rasmi Afisa Michezo, Halmashauri ya Arusha, Priscus Steven amesema kuwa mashindano hayo yamehusisha jumla ya wachezaji 400 kutoka Klasta tano za halmashauri ya Arusha, wachezaji watakaoingia kwenye michuano ya kutafuta wachezaji bora, watakaounda timu zitakazowakilisha halmashauri kwenye mashindano ya UMITASHUMTA mkoa.
Afisa michezo huyo ameongeza kuwa kati ya wachezaji 400, wachezaji 120 tu ndio wanaotakiwa kuchaguliwa na kuunda timu za kuwasilisha halmashauri kwenye mashindano ya mkoa na kuitaja michezo itakayohusika ni pamoja na mpira wa miguu wavulana na wasichana, mpira wa pete, riadha, wavu, mikono, sanaa za maonesho, usafi na nidhamu.
Aidha mashindano hayo yatahusisha michezo kwa watoto wenye mahitaji maalumu, kwa kushiriki kwenye michezo ya riadha maalum, mpira wa miguu maalumu na mpira wa kengele.
Simon Mollel, mwalimu wa kitengo maalum, shule ya msingi Ilboru amesema kuwa, wanafunzi wenye mahitaji maalumu watashiriki na wenzao mashindano hayo huku akieleza kuwa, watoto hao wanauwezo mkubwa na wameandaliwa vizuri kushiriki michezo kama ilivyo kwa watoto wengine.
Mwanafunzi Patrick Fredrick kapten wa timu ya miguu klasta ya Oldonyosambu, amethibitisha kuwa michezo inaongeza mahudhurio ya wanafunzi shule kwa kuwa wakimaliza muda wa masomo wanaingia kwenye michezo.
Hata hivyo Patrick ameelezea changamoto ya ukosefu wa viwanja kwa baadhivya shule na shule nyingibkuwa na viwanja visivyo na viwango na vingine kuharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mashindano ya UMITASHUMTA mwaka 2018, yalianza mapema mwezi Februari ngazi ya shule, kata mpaka klasta, halmashauri, mkoa na yanategemea kuhitimishwa mwezi Juni kwa ngazi ya taifa , mashindano yenye kauli mbiu ya "Michezo, Sanaa na Taaluma ni Msingi wa Maendeleo ya Mwanafunzi katika Taifa Letu"
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.