Kufuatia migogoro ya ardhi inayotokana na matumizi yasiyo rasmi na kusababisha hasara kwa jamii na taifa, Tume ya taifa ya kupanga matumizi bora ya ardhi imeanza kuwajengea uwezo watalamu wa halmashauri juu ya matumizi bora ya ardhi kwenye ngazi za vijiji.
Baada ya kujengewa uwezo, watalamu hao watakwenda kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vyote ndani ya halmashauri ya Arusha ili kuwa na ardhi bora iliyopangwa na kutunzwa kulingana mahitaji ya jamii husika.
Mkurugenzi msaidizi Tume ya taifa ya kupanga matumizi bora ya ardhi, Albina Bura amesema kuwa suala la kupanga ardhi ni suala mtambuka linahitaji ushirikishwaji wa watalamu fani mbalimbali watakaowezesha kupanga ardhi kulingana na matumizi ya eneo husika na uhitaji wa jamii.
Amesisitiza kuwa mipango bora, ya matumizi bora ya ardhi, yanatakiwa kuanzia ngazi ya vijiji kule ambako bado ardhi haijavamiwa kwa kiasi kikubwa.
Ameongeza kuwa kutokana na ongezeko la watu linalosababisha uhitaji mkubwa ardhi, ardhi inatakiwa kutunzwa na kupangwa kwa ajili ya vizazi vijavyo kwa kuwa ardhi haiongezeki.
"Ni vema kupanga matumizi bora ya ardhi vijijini, ili ardhi hiyo iweze kutumika kwa wakazi wote kulingana na shughuli halisi za jamii bila kuathiri mazingira" amesema Bura
Aidha ameongeza kuwa jamii inapaswa kukubali kutumia ardhi kulingana na mipango ya matumizi ya ardhi, mipango itakayoandaliwa kitaalamu kulingana na mahitaji ya jamii husika.
Bura amezitaka halmashauri kuanza kupanga ardhi kwenye vijiji ambavyo ukuaji wake unadalili za kuwa miji ili jamii ikute tayari kuna mpango wa matumizi bora ya ardhi hiyo.
Afisa Mifugo halmashauri ya Arusha Epifania Swai amesema kuwa kuna bado kuna tatizo la wafugaji kufuga mifugo mingi kuliko eneo, jambo linalosababisha uharibifu wa mazingira hasa ardhi na kuongeza kuwa kupitia mafunzo hayo halmashauri itaendelea kuhamasisha na kutoa elimu zaidi kwa jamii ya wafugaji ili waweze kupunguza mifugo na badala yake kufuga mifugo michache yenye tija.
Naye Afisa Kilimo, Elisha Sanari amesema kuwa mpango bora wa ardhi utawezesha kutumia ardhi ndogo kulima, kufuga na hata makazi tofauti na sasa kilimo na mifugo vinafanyika bila mpango.
Hata hivyo jamii inapaswa kufahamu kuwa ardhi ni rasilimali yenye thamani kubwa na isiyoongezeka licha ya kuwa watu wanaongezeka na wanahitaji kutumia ardhi hiyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.