Wanafunzi shule ya sekondari Mwandet, halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru, wanategemea kuanza kutumia bwalo lao la chakula, baada ya serikali kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi bwalo hilo, bwalo ambalo wanafunzi hao wamekuwa wakilisubiri kwa muda mrefu.
Wanafunzi hao, ambao kwa sasa hawana sehemu maalumu ya kulia chakula, jambo ambalo linawapa usumbufu mkubwa kwa kula chakula nje wakiwa wamesimama au kukaa katika maeneo yasiyo rasmi kwenye maeneo ya shule.
Akizungumza na mwandishi wetu, alipotembelea shuleni hapo, mkuu wa shule ya sekondari Mwandet, mwalimu John Masawe, amesem kuwa, wamepokea fedha kutoka Serikali Kuu, za miradi ya P4R, kiasi cha shilingi milioni 100, fedha ambazo kiasi cha shilingi milioni 50 kinatumika kumalizia ujenzi wa bwalo la chakula huku milioni 50 nyingine zikianzisha ujenzi wa maktaba.
Mwalimu Masawe amekiri kuwa, ukamilishaji wa bwalo hilo la chakula, utaondoa adha kubwa wanayoipata wanafunzi wakati wa kula, kwakuwa husimama na kukaa nje, mazingira amabyo si rafiki wala salama kiafya, kutokana na hali ya hewa ya eneo hilo ya upepo unaombatana na vumbi, wakati wa jua na baridi kali na wakati wa mvua pia, hali zote huwapa usumbufu mkubwa wanafunzi hao.
Ameongeza kuwa, licha ya kuwa hali ya hewa ni changamoto kubwa, kitendo cha kulia nje kinaenda sambamba pia na uchafuzi wa mazingira, jambo ambalo linatishia usalama wa wanafunzi kiafya.
Hata hivyo mwalimu Masawe, amethibitisha kuwa, fedha hizo zinatosha kutakamilisha ujenzi wa bwalo hilo na wanategemea likamilike na kuanza kutumika mapema mwishoni mwa mwezi Machi kwa kuwa fundi anayefanya kazi hiyo anakwenda vizuri.
Amezitaja kazi zinazofanyika ni pamoja na uwekaji wa sakafu na malumalu, milango na madirisha, upakaji wa rangi kwa jengo zima, uwekaji wa majiko matatu ya kisasa pamoja na meza na viti vya kukalia wanafunzi hao wakati wa kula.
Salhat Adam, mwanafunzi wa kidato cha kwanza anashukuru serikali kwa kuwajengea bwalo, kutokana na adha wanayoipata kwa kula chakula nje, jambo ambalo linatishia usalama wa afya zao.
Akizungumzia upatikanaji wa chakula shuleni hapo, mkuu huyo wa shule amesema kuwa, kwa wanafunzi wa bweni wa kidato cha tano na sita serikali inatoa chakula, kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha nne wa bweni na kutwa, wanagharamiwa na wazazi kwa makubaliano ya wazazi wenyewe.
Hata hivyo, mkuu huyo wa shule, amesema kuwa bado kuna changamoto kwa wanafunzi wa kutwa, ambao baadhi ya wazazi kushindwa kuchangia chakula cha watoto wao, na kuwasababishia watoto hao kushinda na njaa wawapo shuleni.
Amewataka wazazi hao kujitoa, kuwalipia watoto wao fedha ya chakula kwa kuwa licha ya kuwa ni jukumu lao, lakini ni kwa ajili ya afya na maendeleo ya watoto wao, kutokuwalipia ni kuwanyanyasa kisaikolojia, hata maendeleo yao darasani huwa ni ya kusuasua.
"Wazazi waoneeni huruma watoto wenu, walipieni chakula, mtoto anakaa shuleni muda mrefu na njaa, anapoona wenzake wanakula yeye hali, ananyanyasika sana, hata maendeleo yake darasani yanasuasu. Amesema Mwalimu Masawe.
Shule ya sekondari Mwandet ilianza mwaka 2004, na mwaka 2016 ikipandishwa hadhi na kuwa na kidato cha 5 na 6, na ina jumla ya wanafunzi 1,232 kidato cha kwanza mpaka cha sita.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.