Watumishi wa halmashauri ya Arusha, wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ya kuwahudumia wananchi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, ili kuleta tija na maendeleo katika halmashauri hiyo.
Akizungumza na watumishi hao, alipokutana nao kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, amesema kuwa, jambo kubwa litakalosaidia kuleta maendeleo kwa wananchi wa halmashauri ya Arusha ni uwajibikaji wenye tija na moyo wa kujituma bila kuchoka.
Dkt.Mahera ameongeza kuwa, jukumu kubwa la watumishi wa umma ni kuwahudumia wananchi bila kujali hali zao wala itikadi zao, kwa kuwa ni haki ya kila mwananchi kupata huduma bora anayohitaji, hali ambayo itajenga imani kwa wananchi.
" Kila mwananchi anahaki ya kuhudumiwa na kupata huduma bora na sahihi anayohitaji bila kujali hali yake ya kiuchumi, itikadi zao za kidini wala za kisiasa" amesisitiza Mkurugenzi Mahera.
Hata hivyo, Dkt. Mahera amewataka wakuu wa Idara na Vitengo, kuwasimamia watumishi wote walio chini yao na kuhakikisha wanatekeleza majukumu ya pamoja na kusimamia miradi yote ya maendeleo, inayotekelezwa chini idara na vitengo vyao bila kutoa wala kupokea rushwa.
"Niwatake wakuu wote wa Idara na Vitengo, kuwajibika vizuri na kuhakikisha mnawasimamia watumishi walio chini yenu huku mkisimamia vyema miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Idara na Vitengo vyenu, na kuacha tabia ya kupokea rushwa" amesema Dkt.Mahera
Kadhalika, Mkurugenzi Mahera, amemtaka Afisa Utumishi wa halmashauri hiyo, kuhakikisha kila idara inatekeleza majukumu yake kwa ufasaha pamoja na kutenga muda maalumu wa kusikiliza matatizo ya wananchi.
Kwa upande wake Afisa Utumishi wa halmashauri ya Arusha, Mohammed Mavura, ameahidi kushirikiana na watumishi wa ngazi zote ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuleta maendeleo katika halmashauri yao.
Afisa Utumishi huyo pia, amewataka watumishi wote kufanya kazi kwa ushirikiano huku nidhamu ya kazi ikiwa ni kipaumbele na kuongeza kuwa, Idara ya Utumishi haitawahurumia, watumishi ambao hawatatekeleza majukumu yao vizuri kwa mujibu wa sheria za kazi.
"Nitakuwa mtu wa kwanza kumshauri mkurugenzi kumshughulikia mtumishi yeyote ambaye, hatatekeleza majukumu yake ipasavyo" amesema Mavura
Halmashauri ya wilaya ya Arusha ni moja kati ya halmashauri yenye mkakati wa kutekekeza kwa vitendo, juhudi za serikali ya awamu ya tano kwa kufanya kazi kwa bidii, kupiga vita rushwa pamoja na kutoa huduma kwa kuzingatia haki sawa kwa wananchi wote.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.