Wauguzi halmashauri ya Arusha, wameungana na wauguzi wenzao duniani, kuadhimisha siku ya Wauguzi duniani huku halmashauri yao ikiwa na mafanikio makubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya afya katika vituo vyake vya kutolea huduma za afya katika maeneo ya pembezoni.
Kama inavyofahamika, mazingira bora ya kazi ikiwemo ubora wa miundombinu na uwepo wa vifaa tiba katika maeneo ya kutolea huduma za afya, humuwezesha muuguzi kufanya kazi yake kwa kujiaamini na kwa weledi zaidi.
Hata hivyo wauguzi hao wamekiri kwa njia ya wimbo kwa kuthibitisha kuwa, wao hujisikia wanyonge pindi mgonjwa anapofika hospitali kupata huduma na huduma hiyo kukosekana katika eneo hilo la kazi.
Akihutubia wakati wa maadhimisho hayo, mgeni rasmi na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, amekiri kuwa, halmashauri ya Arusha inaadhimisha siku ya wauguzi duniani huku ikiwa na mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya vituo vya afya kwenye maeneo ya pembezoni ya kata za Nduruma, Mlangarini na Bwawani, kata ambazo kwa muda mrefu, wananchi wake wamekuwa wakiteseka kutafuta huduma hizo, kwa umbali wa zaidi ya kilomita 30.
Mkurugenzo huyo, ameongeza kuwa, licha ya uboreshaji wa vituo hivyo vya afya kuwanufaisha wananchi wa maeneo hayo lakini pia unawarahisishia wauguzi kutoa huduma kwa wagonjwa na wateja wao kwa ufanisi na weledi.
Amefafanua kuwa jumla ya vituo viwili vya afya, vimeboreshwa na kuwa na sifa ya nyota tano katika kata ya Nduruma na Mlangarini kwa kukarabati na kuongeza majengo, kwa ajili ya upanuzi wa utoaji wa huduma zote muhimu.
Amevitaja vituo hivyo ni pamoja na kituo cha afya Nduruma kilichogharimu shilingi milioni 500 na kituo cha afya Manyire, kinachomaliziwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kwa gharama ya shilingi milioni 190.
Aidha Dkt. Maera ameendelea kusema kuwa, vituo hivyo vyenye hadhi ya nyota tano, vitatoa huduma za wagonjwa wa nje na wakulazwa, huduma za uzazi, kliniki ya mama na mtoto, upasuaji na huduma za maabara.
Amewahakikikishia wauguzi na wananchi wa maeneo hayo kuwa, tayari serikali imeshaagiza vifaa tiba kwa ajili ya kituo cha afya Nduruma vyenye thamani ya shilingi milioni 220 kutoka Bohari kuu ya Dawa 'MSD' na muda mfupi vitawasili na kuanza kuwapatia huduma.
Licha ya kuwepo na vituo hivyo viwili vya afya kwa maeneo ya pembezoni, Mkurugenzi huyo ameweka wazi kuwa, kwa sasa halmashauri imeanza kutoa huduma ya Mkoba 'mobile clinic' kupitia gari la kutolea huduma za dharura ambalo wahudumu wa afya huwafuata wananchi katika maeneo yao, aidha kipaumbele cha matumizi ya gari hilo yamewekwa kwenye maeneo ya pembezoni hasa maeneo ya kata za Oldonyowas, Oldonyosambu na Olkokola, Bwawani, Oljoro na Laroi pamoja na maeneo mengine itakapohiajika huduma ya dharura.
Hata hivyo, Wauguzi hao, wameadhimisha siku yao rasmi huku halmashauri ikifanya vizuri kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii 'CHF' na kuwa halmashauri ya kwanza kati ya halmashauri 7 za mkoa wa Arusha, kwa kufikisha asilimia 50.3% , hivyo wananchi wake, kuwa na uhakiki wa matibabu pindi wanapougua, huku serikali ikielekea kuimarisha mfuko huo na kuwa na Mfuko wa ya Jamii ulioboreshwa, itakayowawezesha kutibiwa kuanzia Zahanati mpaka hospitali ya mkoa.
Ameendelea kufafanua kuwa halmashauri kupitia mapato yake ya ndani, imewakatia vitambulisho vya 'CHF' wazee 692 na kuwahakikishia matibabu rahisi na ya haraka, kwa kuwa na dirisha la wazee kwenye vituo vya afya na hospitali zenye idadi kubwa ya wagonjwa.
Ndani ya halmashauri hiyo kumejengwa hospitali ya kimataifa ya Maternity Africa katika eneo la Ngaramtoni ya Chini, hospitali itakayotoa huduma bure za mama na mtoto pamoja na matibabu ya ugonjwa wa Fistula.
Wauguzi hao pia wamesherehekea siku yao, huku serikali ya awamu ya tano ikiongeza bajeti ya dawa mpaka kufikia bilioni 639 kutoka bilioni 29 ya hapo awali, jambo litakalowawezesha wauguzi kutoa hudumia kwa kujiamini kwa wagonjwa na wateja wao.
Wauguzi halmashauri ya Arusha wameadhimisha siku hiyo kwa kutoa huduma zaidi ya 10 bure kwa siku nne kabla ya kufikia kilele cha siku hiyo tarehe 12 mwezi Mei, kwenye kituo cha Afya Nduruma huku wananchi wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo.
Muuguzi mkuu, halmashauri ya Arusha Sista Agusta Komba amesema kuwa, mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kutokana na uhaba wa huduma hizo katika maeneo hayo na kuongeza kuwa wananchi wamejitokeza kwa wingi katika siku zote nne na wamepata huduma hizo na muda si mrefu watakadhi ofisi ya kijiji idadi kamili ya watu walihudumiwa kwa siku hizo.
Yohana Faustine moja ya wagonjwa aliyefika kupata huduma siku hiyo amesema kuwa, wamefurahishwa na huduma za bure zilizotolewa kituoni hapo huku akithibitisha sherehe kama hizo hazijawahi kufanyika katika maeneo yao, wamekuwa wakizisikia kwenye vyombo vya habari, na kuishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuwajali wananchi wa vijijini wa hali ya chini kama wao.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.