Wauguzi na watabibu halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru, wameatakiwa kutoa huduma za afya kwa wagonjwa, kwa kuzingatia weledi, maadili na miiko ya taaluma zao, ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwahudumia wananchi wanyonge.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya kitaifa ya 'JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA' katika halmashauri ya Arusha, kampeni yenye lengo la kutokomeza vifo vya mama na mtoto, vitokanavyo na uzazi.
Mkuu huyo wa wilaya, amewataka wahudumu wote wa afya katika halmashauri hiyo, kuwahudumia wagonjwa kwa kuzingatia maadilo huku, wakiwa na tabasamu na bashasha la moyo, kwani kwa kufanya hivyo kunawapa wagonjwa matumaini ya kupona kabla ya kupata huduma nyingine za kitabibu zinazohitaji utalamu zaidi.
"Mgonjwa anapofika hospitali, jambo la kwanza anahitaji faraja, faraja inayotokana na tabasamu lako, pindi unapompokea, tabasamu inampa mgonjwa matumaini ya kupona haraka, kabla ya kupatiwa huduma nyingine za vipimo na dawa, wauguzi mtusaidie kufanya jambo hilo, halihitaji maarifa makubwa ni moyo wa kujitolea " amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha amewaonya wauguzi, kuacha tabia ya kutumia muda mwingi kwenye simu za mkononi kwa kuchati, wakati wawapo kazini,jambo linalowakwaza wagonjwa, badala yake kutumia muda huo kuwasikiliza na kuwahudumia wagonjwa na kuongeza kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha huduma za afya, hivyo jukumu lao kubwa ni kuwahudumia wagonjwa wa aina zote.
"Natoa onyo kwa wahudumu wa afya kuacha tabia ya kuchart muda wa kazi, tunawafuatilia na hatutasita kuwachukulia hatua za kinidhamu, watumishi wanaokiuka taratibu za kazi, kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao" amesema Muro.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, amethibitisha hatua kubwa iliyofikiwa katika halmashauri yake katika sekta ya afya, kwa kuboresha miundombinu ya afya na uwepo wa dawa na vifaa tiba katika halmashauri hiyo, na kuwataka wahudumu wa afya kuwajibika kutoa huduma bora za afya katika maeneo yao ya kazi.
Naye Mganga Mkuu, Halmashauri ya Arusha, Dkt. Peter Mboye, ameweka wazi kuwa, chanzo cha vifo vya uzazi ni kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha mimba na wajawazito kuchelewa kufika hospitali wakati wa uchungu, na kuongeza kuwa, ili kukabiliana na uzazi pingamizi, halmashauri imejipanga kukabiliana na changamoto hizo, kwa kuelimisha jamii kuwawahisha wajawazito kufika vituo vya afya waonapo dalili za uchungu, pamoja na kukusanya damu salama kutoka kwa kuwahamasisha wananchi kujitolea damu.
Muuguzi Mkuu, halmashauri hiyo, Sista Agusta Komba, amesema kuwa, licha ya vifo vya mama na mtoto kupungua, bado mila na desturi za jamii ni changamoto kwa uzazi salama, kutokana na wajawazito kuendelea kujifungulia nyumbani kwa wakunga wa jadi, huku wanaume wakiwa kikwazo cha kutokuhudhuria Kliniki pindi wenza wao wanapokuwa wajawazito.
Awali, Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama, inasisitiza mama mjamzito akivuka Salama, mtoto atavuka salama, Familia itavuka salama na nchi itavuka salama.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.