Na mwandishi wetu
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango amewaagiza wataalam wa halmashauri ya Arusha kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miundombinu ya vituo vya Afya ndani ya siku 7 ili vituo hivyo vianze kuwanufaisha wananchi kwa kutoa huduma zilizokusudiwa katika maeneo husika na kupisha utekelezaji wa miradi mingine ya serikali.
Mhandisi Ruyango ameyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara ya kutembelea na kukagua ukamilishaji wa miundombinu ya vituo vya afya vya Mwandet na oldonyosambu vilivyo jengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu ambapo hadi sasa baadhi ya majengo ya vituo hivyo yapo kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji.
“Niwatake viongozi wote pamoja na watumishi mfanye kazi kwa kushirikiana kila hatua ili kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia matumizi mazuri ya fedha za Serikali ili wananchi wa maeneo haya waweze kuona manufaa ya majengo haya kwa kupata huduma na kuwapunguzia adha ya kutafuta huduma za afya katika maeneo ya mbali”. Amesema Mhandisi Ruyango.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwashukuru wajumbe wa kamati za ujenzi zilizoundwa katika vituo hivyo kwa kufanya kazi nzuri kwa kuwa ni kazi ya kujitolea bila malipo na kuwataka viongozi wa serikali kuendelea kuwapa ushirikiano katika kazi zote ili ujenzi wa miundombinu hiyo uweze kukamilika kwa wakati.
Aidha katika kituo cha Afya cha Mwandet, ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi milioni 740 zilizotolewa na Serikali kuu kwa awamu nne tofauti kwa ajili ya kujenga jengo la mama na mtoto, jengo la OPD, jengo la mionzi, jengo la maabara, jengo la nyumba ya watumishi (3 in 1) pamoja na jengo la kufulia, hadi sasa jengo lililokamilika kwa asilimia zote ni jengo la OPD huku majengo mengine yakiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya kichama ya Meru Mhe. Noel Severe amesema kuwa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya Afya ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi hivyo ni wajibu wa watumishi kushirikiana na viongozi wa chama katika kutekeleza miradi hiyo.
“Ni adhima ya Serikali ya awamu ya sita pamoja na Chama Cha Mpinduzi kupitia ilani yake kuhakikisha tunaboresha na kujenga mazingira mazuri ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, hivyo wasimamizi wa miradi hii hawana budi kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati uliopangwa ili vituo hivi vianze kazi mara moja”. Amesisitiza Mhe. Noel Severe.
Hata hivyo katika kituo cha Afya cha Oldonyosambu, ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali kuu kwa awamu mbili tofauti kwa ajili ya kujenga jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji, jengo la RCH, jengo la mionzi, jengo la kufulia, jengo la maabara pamoja na jengo la nyumba ya mtumishi ambapo hadi sasa jengo lililokamilika kwa asilimia zote ni jengo la RCH huku majengo mengine yakiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Awali, kitu cha afya Oldonyosambu kinahudumia wananchi zaidi ya elfu saba kwa mwaka ambapo miradi hiyo yote itakapokamilika itawapunguzia wananchi wa maeneo hayo pamoja na vijiji Jirani changamoto ya kupata huduma ya vipimo vya X-Ray na vipimo vya maabara sambamba na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.