Na Elinipa Lupembe
Maafisa watendaji wa kata 8 halmashauri ya Arusha wamekabidhiwa pikipiki zilizotolewa na serikali kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi nchini.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pikipiki hizo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi amesema kuwa pikipiki hizo ni vifaa muhimu kwa Maafisa hao zinazokwenda kumaliza changamoto ya kutembea umbali mrefu kuwafikia wanachi ili kutoa huduma.
Ameweka wazi kuwa, kata hizo 8 ziko maeneo ya pembezoni zikiwa na maeneo makubwa ya kiutendaji hivyo Maafisa hulazimika kutembea muda mrefu kuwafikia wananchi kutoa huduma jambo ambalo linakwenda kumalizika sasa.
Aidha amewataka Maafisa hao kutumia pikipiki hizo kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa na serikali ya kuwahudumia wananchi na si vinginevyo huku akiwasisitiza kuzitunza na kuzithamini kwa kutambua kuwa ni mali ya Umma.
"Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuwatahamini Maafisa Watendaji wa kata, kwa kuwa wao ndio wanawahudumia wananchi moja kwa moja, Watendaji mnalo deni sasa, mkatumie vifaa hivi kulingana na malengo yaliyokusudiwa na si kwa matumizi binafsi". Amesisitiza Mkurugenzi Msumi
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya kichama Arumeru, Komredi Noel Severe, ameipongeza serikali kwa kuteketeleza Ilani ya Chama hicho kwa vitendo, kwa kuhakikisha watumishi wanapata vitendea kazi vitakavyorahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.
"Serikali inawategemea, mmepata usafiri, tumieni muda mwingi kutatua kero na changamoto za wananchi kwenye maeneo ya vijiji na vitongoji vyenu kwa wakati, kwa kufanya hivyo, tutafikia malengo ya serikali ambayo ndio maagizo ya Ilani". Amesisitiza Mwenyekiti huyo wa CCM
Hata hivyo Maafisa Watendaji hao, wameipongeza serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwapatia usafiri, jambo ambalo wamekiri lilikiwa ni changamoto kubwa iliyokwamisha utendaji kazi katika maeneo yao.
Afisa Mtendaji wa kata ya Oldonyosambu, Lomnyaki Ndiyogi licha ya kuipongeza serikali amekiri changamoto ya kutembea umbali mrefu wa takribani Kilomita hamsini, jambo lililowafanya kutumia zaidi ya masaa nane kufanya kazi moja.
"Kupitia pikipiki hizi zinakwenda kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu, jambo la kufanya siku nzima sasa tutatumia saa moja, tunamshukuru Mama Samia na tunaahidi kuwahudumia wananchi kwa kasi kubwa sasa". amefafanua Lomnyaki.
Halmashauri ya Arusha ni miongoni mwa halmashauri nchini iliyopata pikipiki 8 kati ya pikipiki 916 zilizotolewa na serikali na kuzigawa kwa Maafisa wa kata za pembezoni za Bwawani Oljoro, Laroi, Musa, Oldonyowas, Oldonyosambu Lemanyata na Sambasha.
Arusha DC
KaziInaendelea✍✍
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MAKABIDHIANO YA PIKIPIKI
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.