Na. Elinipa Lupembe.
Shirika lisilo la kiserikali la Center for Women, Children and Youth Development la Arusha, limeanzisha programu maalumu ya kutoa elimu ya ukatili kwa watoto, katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya COVID 19, kwenye kata za halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru.
Imeelezwa kuwa programu hiyo maaluu, itatekelezwa kwenye kata 17 kwa kuwashirikisha Maafisa Watendaji wa kata, waendesha Bodaboda, watoa huduma za afya ngazi ya jamii na watalamu wa halmashauri ya Arusha kisekta, lengo likiwa kuelimisha jamii kupambana na ukatili dhidi ya watoto katika kipindi hichi ambacho jamii iko kwenye taharuki ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo maalumu, iliyoambatana na mafunzo kwa watalam hao,Mratibu wa Mradi shirika la CWCD Fatuma Ally, amesema kwamba, uanzishwaji wa programu hiyo, umekuja baada ya kuripotiwa kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, vinavyoendelea kwenye jamii, wakati jamii imejikita kwenye kupambana na ugonjwa wa Corona.
Fatuma ameeleza kuwa, katika kipindi hiki cha likizo maalumu kwa ajili ya Corona, kipindi ambacho watoto wako nyumbani, imeripotiwa kuna baadhi ya watoto wa kike wamepata ujauzito, wengine wakiozwa na wengine wamekuwa wakiingiliana kimwili ndani ya familia moja, hivyo ni vema kutoa elimu kwa jamii ya kuzuia ukatili huo wakati wakikabiliana na gonjwa la Corona.
"Tumeshuhudia matukio ya ukatili kwenye vyombo vya habari, huko Tunduru karibia watoto 100 wamepata ujauzito, lakini familia nyingine mzazi anaomba ushauri mtoto wa kiume amewapa mimba dada zake, shirika limeona njia pekee ni kutoa elimu kwa jamii, ili kuondokana na tatizo hilo "amesema Mratibu huyo wa Miradi CWCD.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii, halmashauri ya Arusha, Angela Mvaa, amethibitisha kuripotiwa kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na watoto kuolewa, visa ambavyo vimetokea kipindi hiki ambacho serikali, ilichukua hatua ya kuzifunga shule ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Amewataka Maafisa Watendaji wa kata hao, kufuatilia watoto walioko nyumbani, kama wako salama na endapo kuna watoto wamefanyiwa ukatili watoe taarifa haraka, kwa kuwa tayari kuna fununu ya baadhi ya wazazi wameanza kuwaozesha watoto wa kike.
"Serikali inafahamu idadi ya watoto waliokuwa shuleni, hivyo Watendaji wa kata pitieni maeneo yenu, kuhakikisha watoto wote wako salama na watarudi wote shuleni, endapo kuna mtoto, hatapatikana toeni taarifa ili hatua zichukuliwe" amefafanua Afisa huyo.
Aidha Maafisa Watendahi wa kata hizo, licha ya kushukuru kwa mradi huo, wamekiri kuwa na changamoto za ufuatiliaji wa kesi za ukatili dhidi ya watoto, ikielezwa kuwa upelelezi unaendelea na hatimaye kesi kuisha kiholela.
Afisa Mtendaji kata ya Kisongo, Brighton Mwanri, amethibitisha kuwa, amekwishapeleka kesi tatu tofauti kwenye kituo cha polisi, na kesi hizo kupotelea huko, huku watuhumiwa wakiachiwa huru na kupoteza haki za watoto.
Hata hivyo wakati wa mafunzo ya program hayo, shirika la CWCD liligawa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa ajili ya kutumika kwenye Ofisi za Kata hizo,na jumla ya ndoo 17 za kunawia mikono pamoja na dawa kinga za kuulia vijidudu, wakati wa kunawa mikono.
Programu hii ya muda mfupi inatekelezwa na halmashauri ya Arusha na shirika la CWCD kwa ufadhili wa shirika la Foundation for Civil Society la nchini Tanzania na itafanyika kwa kijpindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.