Na Elinipa Lupembe
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF imetekeleza mradi wa ujenzi wa kivuko kitongoji cha Moivo kata ya Moivo halmashauri ya Arusha, changamoto ambayo ilihatarisha maisha ya watu na mali zao wa eneo hilo.
Wakizungumza mara baada ya Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, kuzindua Kivuko hicho, wananchi wa Moivo licha ya kuishukuru TASAF kwa kuwajengea kivuko, wameeleza madhara yaliyowapata kabla ya kuwa na kivuko ni pamoja na watu kuporwa mali zao na vibaka, wanawake kubakwa huku wengine wakinusurika kuuawa na watoto kushindwa kwenda shule hasa wakati wa mvua kwa kushindwa kupita hapo.
Eliamani Shange ambaye ni mnufaika wa TASAF, ameweka wazi kuwa, kuwepo kwa kivuko hicho sasa kumeondoa kero zote hizo, hakuna tena kichaka cha vibaka hapo na kubwa zaidi sasa watoto wanakwenda shule kwa amani, huku kivuko hicho kikitarajiwa kukuza uchumi wa eneo hilo kwa kuwa wafanya biashara wanasafirisha bidhaa zao kwa urahisi tofauti na hapo mwanzo.
"Hiki kivuko kimetusaidia sana kina mama na watoto, lakini pia kimewarahisishia wajasiriamali kusafirisha bidhaa zao, kama unavyoona magari sasa yanapita hapa yamebeba bidhaa mbalimbali, zamani watu tulibeba kichwani, tunaishukuru sana TASAF ni mkombozi wa jamii na mali zao, usafiri ni wa uhakika usiku na mchana" amesisitiza Mwajabu Hassan
Naye Diwani wa kata ya Moivo Mhe. Selina Mollel, ameipongeza serikali kupitia TASAF kwa kuwaondolea wananchi wake kero ya muda mrefu, sambamba na kuwapongeza walengwa wa TASAF kwa kujenga kivuko hicho kwa mikono yao kupitia mpango wa ajira za muda unaowawezesha walengwa kufanya kazi katika miradi hiyo
"Kipekee niwapongeze walengwa wa TASAF, mmefanya kazi kubwa na nzuri, mmesimama imara na kuhakikisha kivuko kimepatikana kama lilivyokuwa hitaji lenu la muda mrefu, mmefanya kazi kwa moyo bila kukata tamaa, hadi ujenzi umekamilika, serikali yetu inahitaji wananchi wazalendo kama ninyi" Amesisitiza Mhe. Selina.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amewataka wananchi hao wa Moivo, kukitunza kivuko hicho ili kidumu na kuwaletea mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, kwa kuwa tayari serikali imetimiza jukumu lake la kuwawekea miundombinu hiyo kazi yao ni kutumia na kutunza na kusisitiza kuwa mama Samia ameupiga mwingi.
"Kuwepo kwa kivuko katika eneo hili, ni chanzo cha maendeleo katikaneneo hili, kitarahisisha kusafirisha mazao, kuasafirisha bidhaa kwa wafanayabiashara na hata suala la wagonjwa litakuwa rahisi, ambulance zitafika sasa hadi nyumbani" amesisitiza Msuimi
Awali mradi wa Kivuko cha Moivo, umetekelezwa na TASAF kupitia programu za ujenzi wa miundombinu na Ajira za muda, kwa gharama ya shilingi milioni 68 huku asilimia 50 ya fedha hizo zikitumika kununua vifaa na asilimia 50 ikitumika kulipa ujira kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini kwa lengo la kuwaongezea kipato.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍
JIANDAE KUHESABIWA
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA UZINDUZI WA KIVUKO CHA MOIVO.
Kutoka kushoto, Mwenyekiti wa usimamizi wa ujenzi CMC, Brazard Mkwizu, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi (katikati) na Diwani kata ya Moivo Mhe. Selina Mollel, wakikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kivuko cha Moivo, Mradi uliotekelezwa na TASAF III awamu ya II
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi akizungumza na wananchi wa Moivo wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kivuko cha Moivo, Mradi uliotekelezwa na TASAF III awamu ya II
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kivuko - CMC Brazard Mkwizu, akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa kivuko cha Moivo
Mwonekano wa kivuko cha Moivo mara baada ya kukamilika, na tayati kimeanza kutumika
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.