Na Elinipa Lupembe.
Shirika lisilo la kiserikali la WAMATA limewaondolea kero ya maji ya muda mrefu, iliyokuwa ikiwakabili wanawake wa kitongoji cha Nyamagana kijiji cha Themiyasimba kata ya Bwawani, sio tu kwa matumizi ya nyumbani bali kwenye zahanati ya Themiyasimba kwa kina mama wakati wa kujifungua.
Shirika hilo limefanikiwa kujenga mradi wa maji kwa kuchimba kisima kirefu, kuweka matanki ya kuhifadhiamaji pamoja vituo vya kuchotea maji kwa gharama ya shilingi milioni 100, mradi utakaowawezesha wakazi wa kitongoji cha hicho na majirani, shule na zahanati kupata maji safi na salama jambo ambalo halijawahi kutokea kijijini hapo.
Wananchi wa kitongoji hicho, wamelishukuru shirika hilo na kuelezea hisia zao, wakati wa uzinduzi wa mradi huo, namna wanawake walivyokuwa wanateseka kupata maji kwa matumizi ya familia lakini zaidi kwenye zahanati ambayo kina mama wajawazito walikuwa wanakosa maji hasa wakati wa kujifungua.
Happy Kaaya, mkazi wa Nyamagana, amesema kuwa, adha ya maji katika kitongoji hicho iliwapotezea wanawake muda mwingi wa kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa 5 kutafuta maji, jambo ambalo lilidhoofisha hali ya afya na uchumi wa familia zao.
"Sisi wanawake tumepata mkombozi, sisi ndio tulikuwa wahanga wakubwa wa ukosefu wa maji, tulitumia muda mrefu kutafuta maji, lakini zaidi tunafuraha pale ambapo maji yamefika kwenye zahanati yetu ya Themiyasimba, hivyo kinamama hatutateseka tena wakati wa kujifungua" Ameweka wazi Happy
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa maji, Mkurugenzi wa shirika la WAMATA, John Tarimo amesema kuwa shirika hilo kwa ufadhili wa shirika la World Server la nchini Marekani, limefanikisha mradi huo wa maji, mara baada ya kuona adha kubwa ya maji iliyokuwa inawakabili wananchi wa Bwawani hususani kijiji cha Themiyasimba.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha amewashukuru wadau wa shirika hilo kwa kutoa huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa Themiyasimba, ikiwa ni utekelezaji wa malengo ya Serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndoo.
"Serikali inathamini kazi zinazofanywa na wadau za kufanikisha vipaumbele vya Serikali, WAMATA mmewezesha kumtua mama ndoo ikiwa ni sera ya Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na mama Samia Suluhu Hassan". Amesisitiza Mkurugenzi Msumi
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Themiyasimba, Mhel Mussa Msengi, ameshukuru kwa mradi huo wa maji, kwa kuwa changamoto ya maji ilikuwa ni tishio kubwa la afya kwa wananchi walio wengi.
"Wananchi walikuwa na uhitaji mkubwa wa maji safi na salama, hivyo tunaomba kama inawezekana, kuongezewa tanki lingine ili maji yawafikie wananchi wengi zaidi katika vijiji vya jirani, kwa kuwa kisima hicho kina maji mengi na ya kutosha ". Amesisitiza Mwenyekiti huyo wa kijiji.
Awali shirika la WAMATA licha ya kutekeleza mradi wa maji, lakini pia limeanza kuwahudumia vijana 10 watakaopewa mafunzo ya ushonanaji na kuchomelea vyuma lengo kuu ni kupambana na ukosefu wa ajira nchini.
ARUSHA DC
TUPO KAZINI✍✍
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA UZINDUZI WA MRADI WA MAJI KITONGOJI CHA NYAMAGANA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.