Na. Elinipa Lupembe.
Wazee wa koo na mila wa kabila la kimasai, maarufu kama Malaigwanani, halmashauri ya Arusha, wamekubaliana kupambana na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaofanyika ndani ya jamii yao.
Wazee hao wamekubaliana hayo, wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyojumuisha Wazee wa mila na viongozi wa dini, semina iliyofanyika kwenye Ukumbi mdogo wa Mwenyekiti, halmashauri ya Arusha.
Wazee hao wamekiri kuwepo kwa vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuthibitisha kuwa vitendo vingine hufanywa na jamii, kutokana na mila na desturi za kabila la kimasaai.
Wamefafanua kuwa, baadhi ya mila na desturi za Kimasai zimepitwa na wakati, hivyo kama jamii, inapaswa kuachana nazo, kwa kuwa hazina faida, bali zina madhara makubwa kwa jamii yao.
Wazee hao wa mila wameongeza kuwa, licha ya kuwa bado mila hizo zinaendelea kufanyika wamethibitisha kuwa, kwa sasa vitendo hivyo vimeanza kupungua kwa kasi kubwa, kutokana na jamii hiyo sasa kupata elimu na kufahamu madhara ya mila hizo pamoja na sheria zinazozuia ukatili huo.
Hata hivyo wazee hao wamekiri kupambana kwa kasi na ukatili huo kwa kuifanya agenda ya kudumu kwenye vikao vyao vya mila, nyumbani na pindi wanapokutana na wananchi.
Katibu Mkuu wa Ukoo wa Mollel Tanzania, Laigwanani Saitabau Namoyo, amesema kuwa upambanaji wa mila potofu zinazowakandamiza mwanamke na mtoto hasa ukeketaji na ndoa za utotoni, imekuwa ni agenda ya kudumu inayozungumzwa kwenye vikao vya ukoo, huku wakiendelea kuelimishana taratibu kuanzia ngazi za familia.
Mkuu huyo wa ukoo ameongeza kuwa, kwa sasa vitendo hivyo vimeanza kupungua sana, kutokana na ukweli kwamba, hata watoto wenyewe wanazitambua haki zao kwa kufundishwa shuleni.
"Tangu serikali ilipoanzisha shule za kata, jamii ya kimasaai imeanza kupeleka watoto wa kike shule, mtoto mwenyewe akirudi nyumbani,tayari anajitambua na kuanza kutuelimisha madhara ya mila zinazowakandamiza hasa kukeketwa na ndoa za utotoni" amesema Laigwanani huyo.
Aidha ameitaka jamii kutokuichukulia jamii ya kimasaai kuwa ni katili, mila hizo wamezikuta na kuzirithi kutoka kwa babu zao, ingawa kwa sasa wametambua madhara ya mila hizo, huku wakiendelea kuelimishana taratibu na kuachana nazo.
Naye Shehe wa msikiti wa Sambasha, Swalehe Jumanne, amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto kwenye nyumba za ibada na kuwaelimisha watoto juu ya haki zao wakati wa vipindi vya madrasa.
Mkurugenzi washirika la Centre for Women and Youth Development (CWCD) Tanzania, mama Hindu Mbwego, amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwashirikisha viongozi hao wa jamii katika kutekeleza mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto kwenye jamii zao.
Ameongeza kuwa viongozi hao wa jamii, wamejengewa uwezo wa namna sahihi ya kupambana na kuachana na mila hizo, na kuwa na uelewa wa pamoja namna ya kuwalinda watoto pamoja na kutoa taarifa pindi matukio ya ukatili yanapotokea.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Arusha, Lovil Nguyaine amesema kuwa, mafunzo hayo yametolewa na halmashauri kwa kushirikiana na ASAS ya CWDC na jumla ya wazee thelathini wamejengewa uwezo wa mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto katika maeneo yao.
Amefafanua kuwa katika kata hizo kumi kila kata imewakilishwa na Laigwanani mmoja na viongozi wa dini wawili kutoka kata za Mwandeti, Olkokola, Sambasha, Laroi, Lemanyata, Ilkiding'a, Kisongo, Musa, Matevesi na Oljoro.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.