Maafisa Watendaji wa kata halmashauri ya Arusha, wameagizwa kushirikiana na watalamu wa Lishe, Afya ya uzazi na Kilimo kuelimisha jamii juu ya masuala chakula na lishe bora pamoja na afya ya uzazi.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe wilaya ya Arumeru, kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Afisa Tarafa ya Moshono, Dominick Njuriwa, wakati wa kikao cha tathmini ya Lishe cha robo ya nne, mwaka wa fedha 2022/2023, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha.
Hata hivyo,maamuzi hayo yamefikiwa mara baada ya kuwasilishwa taarifa ya tathmini ya lishe, iliyoonyesha bado kuna kata 7 zenye changamoto ya watoto wenye utapiamlo unaotokana na lishe duni, huku watendaji wa kata hizo wakitaja changamoto kubwa ni ukame kwa baadhi ya maeneo, uelewa mdogo wa masuala ya lishe na baadhi ya wanaume kutelekeza familia zao.
Mwenyekiti huyo, amewaagiza Maafisa Watendaji wa Kata, kusimamia suala la Lishe na Afya ya Uzazi kwenye maeneo yao kwa kuzifanya kuwa Agenda ya kudumu kwenye vikao vyote vya serikali za vijiji na kata, pamoja na mikutano mikuu ya vijiji, huku wakiwa na programu za kuelimisha jamii kwa kushirikiana na watalamu wa Lishe, Afya ya uzazi na kilimo.
"Kutokana na changamoto ya uelewa, andaeni programu za kutoa elimu kwa wananchi kwa kushirikiana na watalamu wa Lishe na kilimo, lakini fanyeni tathmini ya programu hiyo kwenye vikao vya kata na vijiji, ili iwe endelevu, zaidi bandikeni kwenye mbao za matangazo hali ya utapiamlo kwenye ofisi zenu ili wananchi wafahamu na kuchukua hatua dhidi ya tatizo hili ambalo ni hatari kwa afya za watoto" Amesisitiza Njuriwa
Hata hivyo Maafisa Watendaji hao, wamezitaja changamoto zinazosababisha utapiamlo kwenye maeneo yao ni hali ya ukame unaotokana na ukosefu wa mvua kwa miaka mitatu mfululizo kwa baadhi ya mwaeneo, huku maeneo mengine kukiwa na uelewa mdogo juu ya lishe bora kwa watoto.
Afisa Mtendaji wa kata ya Oldonyowas, Maliaki Lukumay, amesema kuwa katika kata hiyo hudusani kijiji cha Engutukoit kimekuwa na upungufu wa chakula unaotokana na uhaba wa mvua kwa miaka mitatu mfululizo sasa, na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula katika maeneo hayo.
Naye Afisa Mtendaji kata ya Musa, Yustina Mugera, amebainisha kuwa, changamoto kubwa kwenye kata hiyo, hususani kijiji cha Olchorovus ni uelewa mdogo juu ya umuhimu wa lishe bora kwa familia, kwa kuwa wananchi wa maeneo hayo wamejikita kwenye kilimo cha tumbaku, jambo ambalo wanaume wakiuza tumbaku hizo hawazingatii kununua chakula bora kwa familia zao.
"Niombe watalamu wa Lishe na kilimo, tuandae 'task force' ya kufanya kampeni ya kuhamasisha na kuwaelimisha, wananchi umuhimu wa kulima mazao ya chakula, na pengine kununua chakula bora kwa familia zao, kwa kuwa wanaamini zao la tumbaku linalipa zaidi ya kulima mahindi na huo ndio ukweli". Ameweka wazi Yustina
Akiwasilisha taarifa ya tahmini ya Lishe, Afisa Lishe halmashauri ya Arusha, Doto Milembe amesema kuwa, licha ya kuwa hali ya Lishe inaendelea kuimarika nda
ni ya halmashauri hiyo, ameweka wazi bado vijiji 14 kati ya 67 kwenye kata saba zinachangamoto ya watoto wenye utapiamlo.
"Katika robo ya nne, jumla ya watoto 63,244 walifanyiwa tathmini ya lishe, watoto 738 sawa na asilimia 1.16, walikuwa na utapiamlo, huku watoto 52 sawa na asilimia 0.08 walikutwa na utapiamlo mkali na kupatiwa matibabu na huduma za Lishe kwenye vituo vya afya kwa kushirikiana na wadau wa Lishe". Ameweka wazi Afisa Lishe huyo
Hata hivyo mratibu wa Afya ya Uzazi, halmashauri ya Arusha, Bujiku Butolwa, amesema tathmini ya Afya yaw uzazi kwa mama na mtoto, bado kuna changamoto ya wajawazito kuhudhuria Kliniki kwa utaratibu, umezaji wa vidonge vya Folic Acid, kuchelewa kufika vituo vya afya wakati wa kujifungua pamoja na kuacha kuwapeleka watoto kliniki mara wanapomaliza sindano za chanjo.
Mkutano wa tatmini ya lishe hufanyika kila robo ya mwaka ikiwahusisha Maafisa Watendaji wa kata, Watalamu wa Lishe, Afya ya Uzazi na Utawi wa jamii, ukiongozwa naM kuu wa wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Lishe wilaya.
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.