Na Elinipa Lupembe
Katika kukabiliana na changamoto ya baadhi ya watoto kutokupata chakula cha mchana wawapo shuleni kwa shule za kutwa, halmashauri ya Arusha imeandaa sheria ndogo za kuwabana wazazi wasiotoa chakula kwa ajili ya watoto wao.
Hayo yamewekwa wazi wakati wa kikao cha kamati ya Lishe cha kujadili taarifa za Lishe za halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya tatu ya kuanzia mwezi Januari - Machi 2023, kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Katika kikao hicho Idara mtambuka za Elimu, Kilimo, Afya, Maendeleo ya Jamii na Mipango ziliwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za Lishe kwa kipindi cha robo hiyo ya tatu kiseta, huku taarifa Idara za Elimu Msingi na Sekondari zikionyesha bado kuna changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutokupata chakula cha mchana kwa shule za kutwa.
Akitoa ufafanuzi wa taaifa hiyo Afisa Elimu Sayansi Kimu shule za Msingi, Mwl. Boniface Mwang'onda amesema kuwa licha ya juhudi kubwa ya uhamasishaji na utoaji wa wa elimu kwa jamii na wazazi, kati ya wanafunzi 77,574 wa shule 100 za msingi za serikali wanafunzi 51,125 tu ndio hupata chakula cha mchana shuleni na wanafunzi 26,446 hawapati chakula cha mchana sawa na 34%.
Hata hivyo, Mwanasheria na Wakili Msomi Eliasifiwe Kileo, ameweka wazi kuwa, tayari halmashauri imeandaa sheria ndogo, zitakazotumika kuwabana wazazi ambao hawatatoa chakula cha mchana kwa watoto wao wanaosoma shule za kutwa kwa kuzingatia sheria mama ya sera ya elimu ya mwaka 2014 pamoja na taratibu na makubaliano waliyojiwekea wazazi wenyewe kupitia kamati za shule husika.
"Tayari mchakato wa Sheria ndogo za halmashauri umekamilika na kupitishwa na Baraza la Waheshimiwa Madiwani, kwenda ngazi ya mkoa na kusainiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na hatimaye kuanza kutumika rasmi, sheria ambayo itatoa nafasi ya mzazi kushitakiwa Mahakamani kwa kosa la kukaidi kumlipia mtoto wake chakula cha mchana awapo shuleni". Amefafanua Wakili huyo Msomi.
Naye mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, amewataka wazazi kutambua umuhimu wa watoto wao kupata chakula cha mchana wawapo shuleni kwa kuzingatia uhusiano mkubwa wa lishe na taaluma yaani tendo la kujifunza.
"Wazazi hakikisheni watoto wenu wanapata chakula cha mchana wawapo shuleni kwa kuwa ni haki yao ya msingi lakini zaidi kushindwa kufanya hivyo ni ukatili unaoathiri hali ya ujifunzaji kwa mtoto na hudhoofisha uelewa na ufaulu huku ikishusha kiwango cha taaluma shuleni, wazazi watendeeni haki watoto wenu, msisubiri kubanwa na sheria". Amesema Msumi.
Hata hivyo Afisa Lishe halmashauri ya Arusha, Doto Milembe ameeleza kuwa lishe bora huwezesha makuzi ya mwili na akili ya mtoto, na hujenga ubongo wa mtoto na kuchangamsha akili ya mtoto itakayomrahisishia uelewa wa haraka wakati wa kujifunza.
"Jamii inapaswa kutambua suala la lishe kwa mtoto si suala la serikali bali ni wajibu wa mzazi kumpatia mtoto wake chakula bora, kitakachojenga mwili na akili yake na kumpa mtoto uwezo wa kujifunza kwa urahisi, lishe duni husababisha udumavu wa mwili na akili" Amesisitiza Afisa Lishe huyo.
Serikali imebainisha wazi wajibu wa wazazi wa kuwapa chakula cha mchana watoto wao kwa shule za kutwa kupitia Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na Sheria ya Kimataifa ya mtoto namba 22 na mwongozo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2022 inayosisitiza wazazi kutoa chakula cha mchana kwa mtoto nyumbani na shuleni ikiwa ni haki yake ya msingi.
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.