Na Elinipa Lupembe.
Kufuatia changamoto ya ufinyu wa maeneo kwa wakazi wa halmashauri ya Arusha hususani ukanda wa Juu, wametakiwa kufanya kilimo cha nyumbani kwa kutumia mifuko kuotesha mbogamboga kwa matumizi ya nyumbani na biashara pia.
Rai hiyo imetolewa na watalamu wa kilimo wakati wa maonyesho ya Nanenane kanda ya Kaskazini, teknolojia inayopatikana kwenye banda la kilimo, halmashauri ya Arusha, maonyesho yanayoendelea kwenye viwanja vya Themi -Njiro Jijini Arusha.
Afisa Kilimo mboga mboga, halmashauri ya Arusha, Lucy Mvungi amebainisha kuwa, kutokana na ufinyu wa maeneo katika halmashauri hiyo, hususani kwenye ukanda wa juu, wananchi wanatakiwa kutumia teknolojia ya Kilimo cha Nyumbani cha kuotesha mazao ya mbogamboga kwenye mifuko, ambayo ikioteshwa na kutunzwa vizuri ina muonekano mzuri unaovutia kama ule wa maua nje ya nyumba.
Bi Kilimo huyo, amewashauri wananchi, badala ya kuotesha maua mengi kuzunguka nyumba, ni vema wakaotesha mboga za aina mbalimbalo katika neo hilo dogo, ili kupata chakula kitakachokidhi mahitaji ya familia, sambamba na kuipatia familia lishe bora.
"Unapokuwa na bustani ya mbogamboga nyumbani, inakupunguzia gharama za kununua mboga kila siku, lakini inaipa familia yako uhakika wa kuwa na afya bora, kutokana na uhakika wa upatikanaji wa lishe bora inayotokana na mboga za majani". Amefafanua Afisa Kilimo Lucy.
Aidha ameongeza kuwa kilimo hicho ni rahisi, na hakichukui muda mrefu na kusisitiza kuwa mfuko huo wa sulfeti ukitunzwa vizuri una uwezo wa kudumu zaidi ya miaka miwili na mboga zake hukaa miezi 6 mpaka miaka 2 kutegemea aina ya mboga zilizooteshwa.
Amezitaja aina za mbogamboga zinazoweza kuoteshwa kwenye mifuko ni pamoja na spinachi, saladi, sukuma wiki, bitruti, nyanya chungu, mnafu, saro, nyanya, pilipili kali na pilipili hoho.
Karibu banda la Kilimo halmashauri ya Arusha, kujionea teknolojia mbalimbali za kilimo cha kisasa, ikiwemo kilimo cha nyumbani, uchaguzi wa mbegu bora, upatikanaji wa oembejeo za kilimo na mikopo ya matrekta kwa wakulima kuelekea Ajenda 10 -30 Kilimo Biashara.
KAULI MBIU: "AJENDA 10 -30 KILIMO NI BIASHARA 'SHIRIKI KUHESABIWA KWA MIPANGO BORA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI"
PICHA ZA SHAMBA LA NYUMBANI
Banda la Kilimo halmsahuri ya Arusha likiwa limepambwa na bustani nzuri ya mbogamboga zilizooteshwa kwanye mifuko,
Mboga mboga zilizooteshwa kwenye mifuko, kilimo kinachoshauriwa kufanyika nyumbani kwenye eneo dogo
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.