Benki ya CRDB imeikabidhi halmashauri ya Arusha Jenereta lenye ukubwa wa Kv 22 lenye thamani ya shilingi milioni 23.5, kwa ajili ya matumizi ya ofisi za halmashauri hiyo, jenereta ambalo hapo awali lilikuwa likitumiwa na benki hiyo tawi la Sekei, tawi ambalo kwa sasa limefungwa.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Arusha, meneja wa CRDB kanda ya Kaskazini Bi Chiku Issa amesema, Benki ya CRDB imewiwa kutoa jenereta hilo kwa halmashauri kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya benki hiyo na uongozi wa halmashauri ya Arusha.
“Benki ya CRDB imekuwa na ushirikiano mzuri wa muda mrefu, hasa kwa kipindi chote ambacho Tawi la CRDB Sekei likifanya kazi katika eneo hili, Benki ilishirikiana na halmashauri katika mambo mbalimbali ya kuhudumia jamii, kimsingi CRDB kama benki ya kizalendo imeunga mkono juhudi hizo za serikali". Amebainisha Chiku
Aidha ameongeza kuwa Benki ya CRDB inachukulia kwa uzito suala la uwezeshaji wa wa utoaji huduma kwa wananchi kiseka, hivyo inaungana na serikali katika kusaidia jamii kupitia sera ya benki ya kusaidia jamii yaani 'Cooperative Social Responsibility Policy', sera ambayo inaelekeza Benki kutoa asilimia 1 ya mapato yake kila mwaka na kuyaelekeza katika kusaidia jamii kwenye nyanja za elimu, afya, mazingira na uwezeshaji wa mitaji kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Amefafanua kuwa, utoaji wa Jenereta ni mwendelezo katika kutoa huduma kwa jamii ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa wakati wote, hata pale itakapokuwa inajitokeza changamoto ya kukatika umeme kukatika shughuli ziendelee bila kukwama, na kushauri kuwa ile bajeti iliyotengwa kwaajili ya kununua Jenereta sasa inaweza kuelekezwa maeneo mengine kwaajili ya maendeleo ya jamii.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha Mhe. Dkt.Ojung’u Salekwa licha ya kuishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo wa Jenereta, ameweka wazi kuwa jenereta hilo ni muhimu kwa halmashauri hiyo, itakayosaidia kufanyika shughuli za utaji huduma kwa wananchi wakati wote, pindi itakapotokea changamoto ya kukatika umeme na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo katika shughuli nyingine za kijamii.
“Kwa niaba ya mkuu wa wilaya, napenda kuwashukuru sana kwakuwa sasa hapatakuwa na kukwama kwa shughuli kwa ukosefu wa umeme, lakini yote hii ni kutokana na uhusiano mzuri tulio nao kati yenu na sisi, mmekuwa washirika wetu muhimu sana katika shughuli za maendeleo, ni jana tu mlitupatia madawati 50 yatakayosaidia watoto wetu kutimiza ndoto zao na tunacho angalia hapa siyo idadi ya madawati tunayopata, bali idadi ya watoto watakao yatumia. Madawati 50 maana yake mmewawezesha watoto 150 kujifunza huku wakiwa na utulivu”
Awali mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi pamoja na kuishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo wa Jenereta, amebainisha kuwa Serikali kupitia halmasahuri inatambua mchango mkubwa wa benki hiyo katika kuwahudumia wananchi na kutimiza malengo ya Serikali.
“Tuna tambua jitihada zenu kama benki katika kuwahudumia wananchi wetu, mmekuwa mstari wa mbele kwenye masuala ya kijamii, pale tunapowakimbilia kwaajili ya kushiriki kwenye mambo mbalimbali ya elimu na afya, na hii imejidhihirisha wazi leo, tulipowaomba kutuachia kitendea kazi hiki, kifua umeme hakukuwa na kigugumizi na hatimaye leo mmetukabidhi, tunawashukuru kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Mh.Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi”. Amesema Msumi
Hata hivyo baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Arusha wameipongeza na kuishukuru benki ya CRDB kwa kuwapatia Jenereta na kuweka wazi kuwa, itarahisisha shughuli mbalimbali za utendaji kazi hasa kazi za mifumo pale inapotokea umeme umekatika.
“Jenereta ni muhimu sana kwa taasisi yetu, kazi nyingi za kimfumo zinahitaji umeme, kunakuwa na ucheleweshaji wa kazi pale inapotokea umeme umekatika, kuwepo kwa jenereta na mbadala wa umeme, hivyo tunaahidi kuongeza ufanisi katika kazi za kuwahudumia wananchi". Amesema Mtumishi asiyetaka jina lake litajwe.
Arusha DC ni Yetu, Tushirikiane kuijenga
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.