Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mh.Emmauela Mtatifikilo Kaganda amefungua Baraza la Biashara la Wilaya ya Arumeru, kikao cha Baraza hilo kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Arusha. Akizungumza na wajumbe wa Baraza hilo Kaganda amesema kuwa lengo kuu la Baraza hilo ni kujenga ushirikiano mzuri baina sekta ya umma, sekta binafsi pamoja na Serikali na kwamba ushirikiano ukiimalika utakuza uchumi katika sekta zote pamoja na uchumi wa mtu mmojammoja.
“Kuimalika kwa sekta ya biashara ndivyo nchi inavyoimalika kiuchumi, Serikali inaendesha shughuli zake kupitia kodi za wafanyabiashara, ndiyo maana tumeweka juhudi kubwa katika kuhakikisha sekta binafsi inafanya vizuri. Kwahiyo majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi hujenga kuaminiana na kushirikiana ili kuleta maendeleo ya pamoja”, amesema.
Kwa upande wake Afisa biashara wa Halmashauri ya Arusha bwana Emmanuel Mchamungu amesema kwamba baraza hilo linasaidia kutatua changamoto ZA kibiashara na uwekezaji kwa kuhakikisha kwamba biashara zinafanyika katika mazingira rafiki na Serikali inapata mapato yake bila wafanyabiashara kushurutishwa wala kusumbuliwa.
Naye Mwenyekiti mwenza wa Baraza hilo ndugu Wilfred Daniel Mollel amesema Baraza linatumika kuzileta pamoja sekta binafsi na sekta ya umma jambo ambalo halikuwepo hapo awali kabla ya uanzishwaji wa mabaraza hayo nchini.
“Baraza hili linawezesha kufahamu fursa mbalimbali zilizopo katika Wilaya yeti ya Arumeru, tunapokutana hivi pamoja tunajadiliana namna ya kuboresha mazingira ya ufanyikaji wa biashara jambo litakalokuza uchumi wetu kama taifa”, amesema.
Vilevile baadhi ya wajumbe wakapendekeza Serikali kuendelea kutenga maeneo maalum kwaajili ya wawekezaji na wafanyabiashara wenye mitaji kuwekeza ili kuongeza fursa za Ajira kwa Watanzania pamoja na kuongeza makusanyo yatokanayo na kodi rasmi.
Baraza la Biashara ni jukwaa la majadiliano na ushauri kati ya sekta binafsi na sekta ya umma, ambalo lilianzishwa kwa waraka wa Rais Na.1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali Na.39 la tarehe 28 Septemba 2001.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.