Na. Elinipa Lupembe.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, amekabidhi jumla ya tani 4.4 za mahindi na Kilo 290 za maharage kwa kaya 323 ziliathirika zaidi kutokana na mvua kubwa, zoezi lililofanyika kwenye ofisi ya kata ya Olturumet.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo wa chakula, mkuu huyo wa wilaya, licha ya kutoa pole nyingi kwa wananchi,amewataka, kuendelea kushikamana na kusaidiana panapotokea matatizo katika maeneo yanayotuzunguka.
Amesema kuwa, serikali inatambua madhara yaliyoyapata wananchi, licha ya msaada huo mdogo wa chakula, iko kazini kuendelea kufanya marekebisho ya miundombinu ya barabara kupitia TARURA pamoja na kutumia mitambo ya halmashauri.
Aidha amewataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa wakati wa mvua, huku wakiendelea kutunza mazingira, na kuwakemea watu wote wanaoharibu mazingira, kwa kuwa uharibifu huo ndio unasababisha madhara haya mvua zinaponyesha.
"Historia inaonyeshwa kwa kuthibitihsiwa na wazee wa maeneo haya, kuwa zamani mvua zilinyesha kubwa zaidi lakini kutokana na uharibifu wa mazingira kwa sasa mvua ndogo inaleta madhara makubwa sana, wazee wametuomba kuchukua hatua ili kuzuia, madhara haya yasiendele kutokea miaka ijayo, tunaendelea kuchunguza tutachukua hatua". Amesisitiza Mhe. Emmanuela
Amewasihi, watu wote waliojenga na kufanya shughuli za kilimo kwenye miinuko, vilima na vyanzo vya maji, waache mara moja, wasipofanya hivyo Serikali itawaondoa kwa nguvu.
Hata hivyo, viongozi wawakili wa wananchi, wakiwemo waheshimiwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji na Madiwani, wameishukuru serikalipitia ofisi ya mkuu wa wilaya kwa msaada huo wa chakula, msaada ambao ni muhimu kwa wananchi hao waliopata madhara yaliyotokana na mvua kubwa.
"Tunakushukuru Mheshimiwa mkuu wa wilaya, tangu siku ya kwanza mafuriko yalipotokea, hukutuacha umekuwa pamoja nasi na umeenda mbali zaidi kwa kuwaletea wananchi hawa chakula, ambacho wengi wao akiba yao ya chakula ilichukuliwa na kuharibiwa na mvua hizo" Wamesema Viongozi hao
Hata hivyo viongozi hao wawakilishi wa wananchi, wameiomba serikali, kuweka mpango wa madhubuti wa kurekebisha barabara ambazo zimeharibiwa na mvua, barabara nyingi hazipitiki, na kusababisha adha kubwa kwa wananchi katika maeneo mengi.
"Tunashukuru kwa juhudi za serika, kutoa mitambo kuzibua mitaro, tunaiomba serikali, kuongeza nguvu katika kutengenezewa barabara, baadhi ya maeneo hayapitiki na kusababisha mateso makubwa kwa wananchi" Amesisitiza Diwani kata ya Olturumet, Mhe. Joseph Tinayo.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Selemani Msumi, licha ya kutoa pole kwa wananchi hao, amefafanua kuwa kati ya mahindi tani hizo 4.4, Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini imetoa Kilo 3,000 za mahindi na Kilo 290 za maharage huku Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa wilaya imetoa jumla ya Kilo 1,400, madaftari 300 na kalamu 336 kwa wanafunzi 188.
Awali jumla ya kaya 543 zilipata madhara kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia tarehe 23 mwezi Machi, 2023, huku kaya 323 ziliathirika zaidi ndizo zilizopewa msaada wa chakula kutoka kata za Kimnyaki, Sambasha, Olturumet, Olmotony na Oloirieni.
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.