Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda amewaagiza TANROAD, TARURA pamoja viongozi wengine ndani ya Wilaya ya Arumeru kushirikiana kuchukua tahadhari dhidi ya Mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni kwa kurekebisha mitaro inayoelekeza maji kwenye makazi ya watu.
Mhe. Emmanuela amesema hayo wakati akikagua miundombinu ya ujenzi wa barabara ya mianzini, Olemringaringa, timbolo - Ngaramtoni ambapo ambapo amewaagiza TANROAD kushughulikia changamoto za wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo ikiwemo kuwajengulea vivuko vya kuingilia kwao.
"TANROADS warekebishe maeneo ya njia ambazo wananchi wanatakiwa kupita pamoja na njia ndogo ndogo ambazo zinaunganisha barabara hiyo ya lami lakini pia kutengeneza makinga mvua ambayo yatapunguza kasi ya maji kwenda kwenye makazi ya watu ili mvua hizo zisilete madhara kwa wananchi". Ameagiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Hata hivyo, ametoa rai kwa wananchi wote wanaoishi kwenye njia za mikondo ya asili ya maji kuanza taratibu za kuhama maeneo hayo ili kuepusha madhara yatakayoweza kujitokeza na kuongeza kuwa, wilaya ya Arumeru imejipanga vyema kuhakikisha kuwa wanakabiliana na mvua hizo ili madhara yaliyotokea wakati wa kipindi cha mvua zilizonyesha mwezi April yasitokee tena.
Aidha, madiwani kutoka kwenye Kata zilizoathirika na mafuriko ya mvua za masika za mwaka huu wamejitokeza kwa pamoja kujadili namna ya kudhibiti janga hilo kwa kutafta njia bora za kuchepusha maji yanayopita kwenye barabara hiyo kwenye mito iliyokaribu pamoja na kutengeneza makinga mvua kwenye eneo la kitako cha mlima Meru, msitu wa chuo cha Olmotonyi kwani kutokana na ujenzi wa miundombinu ya barabara hiyo inachochea maji kuongezeka na kuelekea kwenye makazi ya wananchi.
"Ujenzi wa barabara hii ni muhimu sana na yenye manufaa kwa wananchi wa Kata hizi hasa akina mama kwani itawarahisishia kufanya shughuli zao za mendeleo ya kiuchumi kutokana na kuwepo kwa usafiri wakati wote, lakini ni vyema kuangalia uwepo wa barabara hii isiwe kero kwa miundombinu yake kuelekeza maji kwenye makazi yao na kusababisha mafuriko". Amesema Diwani wa kata ya Sambasha.
Naye kiongozi wa Mila kijiji cha Timbolo, Laigwanan Raleto Raphael amesema kuwa ni vyema TANROADS kushirikiana na wananchi wakazi wa maeneo hayo kurekebisha maeneo yote mapema ili wananchi waweze kupita kirahisi na kuendelea na shughuli zao za kila siku kabla ya mkandarasi kuondoka kwenye eneo la kazi.
Hata hivyo, Mhandisi wa TANROADS, Hophine Mollel ameahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na wananchi wa kata hizo kwa wakati kabla ya ya mvua hizo kuanza kunyesha.
Awali, wananchi hao waliwasilisha changamoto hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kutokana na ujenzi wa makarvati ya barabara hiyo kuelekeza maji kwenye makazi yao hali ambayo ingeweza kusababisha mafuriko wakati wa mvua.
UJENZI WA BARABARA UENDANE NA MIUNDOMBINU YA MAJI KUZUIA ATHARI ZA MVUA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.