Na. Elinipa Lupembe.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, mheshimiwa Mhandisi Richard Ruyango, ametoa siku 14 viongozi wa vijiji vya Kisimiri Juu, kata la Uwiro halmashauri ya Meru na kijiji cha Losinoni Juu kata ya Oldonyowasi, halmashauri ya Arusha, kukaa vikao na kutoa mapendekezo ya maridhianao lengo likiwa kutatua mgogoro wa eneo la malisho katika mlima Lekishori, eneo linalogombewa na wananchi wa pande hizo mbili.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa siku 14 kwa viongozi hao, baada ya kukutana na wananchi wa vijiji hivyo viwili kwa nyakati tofauti huku kila upande ukionyesha hauna shida na upande mwingine, lakini kila upande ukilalamikia upande mwingine kuwa, ndio chanzo cha mgogoro huo, mgogoro unaohusisha eneo la nyanda ya malisho, wanalodai lililotengwa miaka mingi iliyopita na wazee wao, kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Aidha mheshimiwa Ruyango, amefikia uamuzi huo, baada ya maelezo ya viongozi wa pande zote mbili pamoja na wananchi wao kuweka wazi kuchoshwa na mgogoro huo, mgogoro ambao unawaumiza sana wananchi wa pande zote mbili, kwa kuwa unasababisha kutokuelewana kwa muda mrefu, na kusababisha watu kupoteza mali zao na mtu mmoja kupoteza maisha, huku kila upande ukionyesha ari na matamanio ya kumalizika kwa mgogoro huo ili wananchi hao waweze kuishi kwa amani na utulivu kama ilivyokuwa hapo awali.
Viongozi waliotajwa kukutana na kuleta mapendekezo ya madhiano yao kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ndani ya siku hizo 14, ni pamoja na viongozi wawakilishi wa wananchi wakiwemo wenyeviti wa vijiji vya Losinoni Juu na Kisimiri Juu, Waheshimiwa Madiwani wa kata hizo mbili za Owiro na Oldonyowasi, maafisa watedaji wa vijiji na kata zote mbili, Maafisa Tarafa wa Tarafa hizo mbili pamoja na viongozi wa mila, maarufu kama Malaigwanani wa pande zote mbili.
"Nyinyi viongozi wa wananchi ninawapa siku 14, nendeni mkakae kila kila kijiji na viongozi wake, mkalete mapendekezo ya maridhiano ya nini kifanyike ili kumaliza mgogoro huo, makubaliano hayo yawasilishwe kwenye yangu ndani ya siku hizoo 14, kwa ajili ya utekelezaji wa kukutanisha pande zote mbili, lengo letu kubwa ni kumaliza mgogoro huu, ili muendelee kuishi kwa amani na utulivu, kama yalivyo matamanio yenu nyote mliyotuleza hapa kwenye mikutano" amesisitiza Mkuu wa Wilaya Ruyango.
Hata hivyo viongozi hao wa vijiji vyote viwili vinavyolumbana wamekiri mbele ya mkutano kuwa, wanahitaji kumalizika kwa mgogoro huo wa muda mrefu, mgogoro ambao wamekiri unarudisha nyuma maendeleo katika maeneo yao, kutokana na wananchi wao kutumia muda mwingi kwenye malumbano, badala ya kujikita kwenye mipango ya maendeo.
Viongozi hao licha ya kumpongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kukutana nao na kufanya mikutano nao, mikutano iliyowapa fursa ya kutoa yao ya moyoni, huku wakionyesha uhalisia wa mgogoro huo, na kukubali kukaa kila upande na kuandaa mapendekezo ya maridhiano ndani ya siku hizo 14 walizopewa, huku wakiomba kumalizika kwa mgogoro huo unaotesha wananchi wao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kisimiri Juu, mheshimiwa Mbaiyani Kuresoi. amethibitisha kuwa maamuzi hayo ya mkuu wa wilaya yako sahihi na wao kama viongozi wa wananchi wako tayari kufanyia kazi maagizo hayo, ili kumaliza kabisa tofauti zao, ambapo amekiri kuwa wananchi wa vijiji hivyo viwili kwa asili ni ndugu, hata kabla ya kugawanywa kwa mipaka ya halmashauri hizo mbili za Arusha na Meru.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Losinoni Juu, mheshimiwa Saitoti Ngoilenya, hakuwa tofauti na wananchi wengine, amekiri kutumia fursa hiyo waliyoipata kutoka kwa mkuu wao wa wilaya, kuandaa mapendekezo ya maridhiano ya eneo hilo la malisho, huku wakiweka mbele maslahi ya wananchi wa pande zote mbili, hasa amani na utulivu, unaosababisha kujikita kwenye shughuli za maendeleo na si migogoro tena.
"Tumechoshwa na mgogoro huu, unaokosesha amani wananchi wetu wa pande zote mbili, wananchi ambao kwa asili sisi ni ndugu moja, hatuoni haja ya kulumbana kwa ajili ya eneo ambalo limewekwa na Mungu, na tangu enzi babu zetu walilitunza na kulitumia kwa amani, maagizo ya mkuu wetu wa wilaya tunakwenda kuyafanyia kazi na tunaamini mgogoro huu sasa utafika mwisho " amesisitiza Mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Losinoni Juu.
Awali mgogoro huo, uliodumu kwa zaidi ya miaka mitatu sasa tangu mwaka 2018, unaohusisha kijiji cha Kisimiri Juu kilichoko halmashauri ya Meru na Kijiji cha Losinoni Juu cha halmashauri ya Arusha, ambapo vuguvugu la mgogoro huo lilianza mara baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa halmashauri ya Arumeru na kupata halmashauri mbili za Arusha na Meru, na eneo hilo la malisho kuwa kwenye ramani ya halmashauri ya Meru.
Katika mikutano hiyo, mkuu wa wilaya ya Arumeru aliambatana na mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, mhe. Ojung'u Salekwa, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, mkurugenzi mtendaji halmshauri ya Meru, Zainabu Makwinya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Arumeru.
MATUKIO KATIKA PICHA MKUTANO WA KIJIJI CHA LOSINONI JUU NA KISIMIRI JUU WILAYA YA ARUMERU.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, mheshimiwa Mhandisi Richard Ruyango, akizungumza kwenye mkutano wa wananchi wa kijiji cha Kisimiri Juu kata ya Uwiro, halmashauri ya Meru, wilaya ya Arumeru.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, mheshimiwa Mhandisi Richard Ruyango, akizungumza kwenye mkutano wa wananchi wa kijiji cha Losinoni Juu kata ya Oldonyowasi, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, mheshimiwa Mhandisi Richard Ruyango, akitoa maelekezo kwa viongozi wa mila 'Malaigwanani' wa vijiji vya Kisimiri Juu na Losinoni Juu kwenye mkutano wa wananchi wa kijiji cha Losinoni Juu kata ya Oldonyowas halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru.
Wananchi wa kijiji cha Losinoni Juu kata ya Oldonyowas wakizungumza wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliongozwa na mkuu wa wilaya ya Arumeru, hayupo pichani
Mwananchi wa kijiji cha Kiserian Juu kata ya Uwiro, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliongozwa na mkuu wa wilaya ya Arumeru, hayupo pichani
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.