Na Rlinipa Lupembe
Wazazi halmashauri ya Arusha, wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanapata chakula cha mchana wawapo shuleni, kushindwa kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa juu yao.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda wakati wa kikao cha tathmini ya Lishe cha robo ya pili, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Arusha.
Kufuatia taarifa ya tathmini ya Lishe ya robo hiyo, imeonesha asilimia 78 ya shule huku 50% tu ya wanafunzi ndio wanaopata chakula shuleni, jambo ambalo ni kiashiria hatarishi kwa afya za watoto na zaidi ni kinyume na haki za binadamu.
Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza Maafisa Watendaji wa kata na vijiji kusimamia shule zilizo kwenye maeneo yao na kuhakikisha kila mzazi anawajibika kwa mtoto wake ili apate chakula cha mchana awapo shuleni na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wanaokaidi.
"Tumieni sheria ndogo za vijiji, kuwabana wazazi hao, kwani sera ya Elimu bila malipo imebainisha wazi, moja ya jukumu la mzazi ni kumpatia mtoto mahitaji binafsi ikiwemo chakula, vijiji visivyo na shetia ndogo hakikisheni mnazo ili kuwabana wazazi hao na watoto kupata haki yao ya msingi". Amesisitiza Mkuu huyo wa wilaya.
Aidha amewataka wazazi kutambua umuhimu wa chakula kwa afya ya mtoto, kuwa ndicho kinachojenga akili, mwili na saikolojia ya mtoto, na kuwasisitiza wazazi kuchukulia umuhimu mkubwa jambo hilo.
Akiwasilisha Taarifa hiyo ya tathmini ya Lishe kwa robo ya pili ya mwaka 2022/2023, Afisa Lishe halmashauri ya Arusha, Doto Milembe amesema kuwa mpaka sasa halmashauri inaendelea kufanya vizuri kwenye viashiria 6 kati ya 8 vilivyosainiwa na Maafisa Watendaji wa kata.
Amevitaja viashiria viwili visivyofanya vizuri ni pamoja na idadi ya watoto wanaopata chakula shuleni kuwa ni asilimia 50 tu, jambo ambalo linasababisha kiashiria hicho kupata asilimia ndogo.
"Wazazi kwa kutambua umuhimu wa lishe bora kwa watoto, wanapaswa kutimiza jukumu hilo, kwa kutambua kuwa lishe bora ina nafasi kubwa ya ufaulu wa mwanafunzi katika masomo yake, hivyo tusichukulie ni jambo rahisi hivyo, balibebwe kwa umuhimu wake.". Amesisitiza Afisa Lishe huyo.
Nao Maafisa Watendaji wa kata, wamekiri licha ya juhudi kubwa za ufuatiliaji kwa wazazi kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao, bado kuna changamoto ya uelewa wa baadhi ya wazazi juu ya elimu bila malipo.
Hata hivyo wameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji, kamati na Bodi za shule kuwabana wazazi kutoa chakula na wale wanaokaidi kuchukuliwa hatua za kisheria.
Awali Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha Seleman Msumi, ameahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa viashiria vyote 8 vya lishe ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.
"Tukiangalia tathmini ya robo hii, matokeo yanaendelea kuboreka siku hadi siku, tutaweka mikakati ya kupandisha viashiria hivyo 2 ambavyo bado vina matokeo mabaya". Ameweka wazi Mkurugenzi Msumi
Kikao hicho cha Lishe ni cha kawaida kwa mujibu wa sheria ambapo kila Afisa Mtendaji wa kata anawasilisha taarifa ya Tathmini ya Lishe kwenye kata husika huku ikionyesha utekelezaji na tathmini ya Viashiria 8 vya lishe vilivyowekwa na serikali.
"ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
#KaziInaendelea✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.