Mkuu wa Wilaya Arumeru Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda ametoa maagizo kwa wananchi wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye milima iliyopo Wilayani humo kusitisha mara moja ikiwa na hatua za kuirejesha milima hiyo katika hali yake ya kawaida na kupunguza athari zinazotokana na uharibifu katika milima hiyo ikiwemo mafuriko.
Mhe. Emmanuela ametoa maagizo hayo wakati akitembelea maeneo yaliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na wakazi wanaozunguka mlima huo kufanya shughuli za kilimo na kukata miti ya asili katika Mlima Kivesi Kata ya Sokon II.
Aidha, amesema kuwa kutokana na shughuli hizo za kibinadamu zinazofanyika katika mlima huo kinyume na sheria za Nchi, zimeleta athari kubwa kwa wananchi wengine wanaoishi matika maeneo ya bondeni na kuwataka wananchi hao kuanza kushuka mapema kabla sheria haijachukua mkondo wake.
“Tamko la Serikali leo ni kwamba wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye milima yote ya Wilaya hii ya Arumeru, waanze kushuka na tushirikiane kwa pamoja kurejesha miti kwenye yale maeneo ambayo miti imekatwa”. Amesisitiza Mhe. Emmanuela.
Ameongeza kuwa, kwenye milima yote ya Wilaya hiyo kuna mipaka ambayo imewekwa na Serikali, hivyo haruhusiwi mtu yeyote kuvuka mipaka hiyo na kuwaamuru wote ambao wamevunja utaratibu huo kusitisha kufanya shughuli zozote za kibinadamu kwani kwa kufanya hivyo wanavunja sheria za Nchi.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wanaozunguka maeneo ya mlima huo, wameiomba Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wanavuka mipaka iliyowekwa na Serikali ili kusaidia utunzaji wa mazingira hata kwa vizazi vijavyo.
“kwakweli uharibifu ni mkubwa sana, kuna watu wanaovuta magogo na kusababisha maji mengi kutiririka kuelekea kwenye makazi ya watu, ninaiomba serikali watu hao wasitishwe kuingia kwenye maeneo ya misitu wa asili wabaki kwenye maeneo yao tu”. Amesema mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Ng’iresi kata ya Sokoni II, Maglan Lukumay.
Awali, wananchi wa Wilaya ya Arumeru walishuhudia mafuriko makubwa yaliyosababisha upotevu wa mali za wananchi na wengine kukosa makazi katika msimu wa mvua za mwaka huu, hali iliyosababisha Mkuu huyo wa Wilaya kutembelea maeneo hayo ya mlima Kivesi ambayo yanadaiwa kuwa chanzo kikubwa cha mafuriko hayo ili kushuhudia uharibifu huo.
"ARUSHA DC Ni Yetu, Tushiikiane Kuijenga"
#KaziIendelee
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.