Wasichana yenye umri mdogo wametakiwa kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo kwani wanajiweka kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya magonjwa hatari ikiwemo Saratani ya mlango wa kizazi pampja na gonjwa hatari la UKIMWI.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, na mkuu wa wilaya ya Monduli Mhe. Idd Kimanta wakati wa uzinduzi wa chanjo mpya ya Saratani ya Mlango wa Kizazi katika halmashauri ya Arusha, uliofanyika kwenye hospitali ya wilaya ya Olturumet.
Mkuu wa wilaya huyo amewaasa wasichana kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya ngono, licha ya kupata kinga ya Saratani ya Mlango wa Kizazi na kuongeza kuwa chanjo hiyo haizuii kupata maambukizi ya magonjwa mengine yanayoombukizwa kwa njia ya kujamiiana.
Amefafanua kuwa, vitendo vya ngono katika umri mdogo vinachangia sana kukatisha ndoto za wasichana wengi na wakati mwingine husababisha wasichana wengine kupoteza maisha.
Hata hivyo Kimanta amewataka wazazi, walezi na jamii nzima kuhakikisha wasichana wenye umri wa miaka 14, wanakwenda kupata chanjo hiyo huku akiwataka viongozi wa kata zote kusimamia zoezi hili kwa ufasaha na kuhakikisha hakuna mtoto atakayekosa chanjo hiyo pamoja na kuwaonya watu watakaokwamisha zoezi hilo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Naya mratibu wa chanjo halmashauri ya Arusha Dkt. Yassin Winga , amesema kuwa halmashauri inategemea kuwapatia chanjo jumla ya wasichana 4,239 itakayotolewa kwenye vituo 50 vilivyopo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya halmashauri na zoezi litafanyika ndani ya wiki nzima.
Dkt. Winga amefafanua kuwa, zoezi la chanjo litatolewa pia kwa kutumia 'Mobile Clinic' kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni na kusema kuwa chanjo hii itatolewa mara mbili na mara tatu kwa wasichana wenye maambukizi ya VVU ndani ya miezi sita.
Aidha baadhi ya wanafunzi waliofika kituoni hapo na kupatiwa chanjo hiyo, wamekiri kuridhishwa na chanjo hiyo na kusema kuwa wanaamini chanjo hiyo itawakinga na ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na kukiri kutokujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo.
Asnath Melau msichana aliyepatiwa chanjo amesema kuwa, chanjo waliyoipata ni muhimu kwa maisha ya msichana hasa ukizingatia wanawake wengi hupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kansa ya mlango wa kizazi.
"Hii chanjo ni nzuri na ni muhimu kwetu wasichana, kwa kuwa wakina mama wengi wanakufa na kansa ya mlango wa kizazi, tunashukuru serikali kwa kutupatia kinga na inatupa amani ya kutokupata maambukizi" amesema Asnath.
Hafla hiyo imeambatana na igizo lililohamasisha jamii kuhakikisha wasichana wa miaka 14 wanapata chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi pamoja na upimaji wa afya, lililotolewa na kikundi cha sanaa cha vijana cha ACE AFRICA.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya Kimanta amelishukuru shirika lisilo la kiserikali la ACE AFRICA kwa kujitoa kwa halina mali kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ndani ya halmashauri ya Arusha
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.