Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha Seleman Msumi, amewataka wananchi wa halmashauri hiyo ambao bado hawajahesabiwa, kuondoa hofu kwa kuwa zoezi hilo la Sensa ya Watu na makazi linaendelea mpaka kufikia tarehe 30.08.2022.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Mkurugenzi Msumi, amewasisitiza Wakuu wa Kaya ambao kaya zao hazijafikiwa na Makarani kuhesabiwa na hawatakuwepo nyumbani, kuhakikisha wameacha taarifa zao za msingi nyumbani ili Karani wa Sensa atakapopita akute taarifa hizo.
"Zoezi la Sensa bado linaendelea niwatake wakuu wa kaya kuacha taarifa zao nyumbani, pindi Karani atakapofika atachukua taarifa hizo na Karani atalazimika kukupigia simu na atakapokupigia simu kuhakiki usahihi wa taarifa zako, ninawasihi kupokea simu hiyo na kutoa ushirikiano" Amesema Mkurugenzi Msumi.
Amezitaja taarifa za msingi ambazo Mkuu wa Kaya, anatakiwa kuziacha nyumbani ni pamoja na majina Kamili (majina matatu), idadi wa watu waliolala kwenye kaya na uhusiano wa mkuu wa Kaya na watu waliolala usiku wa kuamkia siku ya Sensa, Jinsi (me/ke), hali ya ndoa ya mkuu wa kaya (ameoa/hajaoa), namba za simu na namba za nida.
Hata hivyo mkurugenzi huyo, amebainisha kuwa, zoezi la Sensa linaendela vizuri, kukiwa hakuna changamoto kubwa iliyojitokeza, na kuongeza kuwa wakazi wa halmashauri hiyo, wanamwitikiao chanya, wakiendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa huku wengi wao wakiacha taarifa zao nyumbani pindi wanapokwenda kwenye shughuli zao za kutafuta riziki.
Zoezi la Sensa ya watu na Makazi linaendelea katika halmashauri ya Arusha, kukiwa na hali ya amani na utulivu, huku wakazi wa halmasahuri hiyo wakiendelea na shughuli zao na kuacha taarifa zinazohitajika nyumbani.
HAKIKISHA UMEHESABIWA✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.