Na Elinipa Lupembe.
Baada ya serikali kutoa fedha za Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19, kwa ajili ya kuboresha wa miundombinu ya shule nchini, wanafunzi wamenufaika kwa kuondokana na msongamano kwenye vyumba vya madarasa.
Shule ya sekondari Ilkiding'a halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru ni miongoni mwa shule za halmashauri hiyo, iliyopokea kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 11 vya madarasa pamoja na viti na meza.
Aidha kukamilika kwa ujenzi wa madarasa hayo, kumewezesha shule hiyo kuwa na vyumba vya madarasa vya kutosha kwa kuwa na uwiano wa wanafunzi 50 kwa kila darasa, uwiano ambao umeondoa kabisa msongamano wa wanafunzi darasani kama ilivyokuwa hapo awali.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Ilkiding'a licha ya kuishukuru serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na mama Samia Suluhu, wamethibitisha kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishiwa, huku wakiahidi kusoma kwa bidii, kwa kuwa serikali yao makini, imewaandalia mazingira rafiki pamoja na kuwapatia elimu bila malipo.
Maurine Philemon mwanafunzi wa kidato cha nne, amekiri kuwepo kwa utulivu wa hali ya juu kwa wanafunzi wakati wa kujifunza na kufundishwa, hali iliyosababishwa na ujenzi wa vyumba 11 vya madarasa shuleni hapo kwa wakati mmoja.
"Kwa sasa tunasoma kwa nafasi na uhuru zaidi, hakuna tena msongamano, kila mwanafunzi anakaa kwenye meza na kiti chake, walimu wanatufundisha kwa kumfikia kila mwanafunzi, tunampongeza mama yetu mama Samia, zaidi tunamuombea na tunaahidi kuongeza juhudi na kufaulu masomo vizuri, kwa kweli hatutamuangusha mama" Amethibitisha Maurine
Hata hivyo wanafunzi hao wameweka wazi kuwa, miundombinu inayovutia shuleni hapo, imewezesha wanafunzi wengi kupenda shule na kupunguza utoro uliokuwepo, huku wakiahidi kuitunza miundombinu yote ya shule, ili iwasaidie wao na vizazi vijavyo.
Naye Mkuu wa shule ya sekondari Ilkiding'a, Mwl. Supeet Sailevu, amesema kuwa, mradi huo pia umesaidia walimu, kwa kufundisha idadi ya wanafunzi darasani kwa wastani unaotakiwa, zaidi yameimarisha upimaji kitaaluma, kwa kuwa wanafunzi wote wanafanya mtihani kwa wakati mmoja sio kwa shifti kama zamani, hali iliyoondoa udanganyifu na kupandisha taaluma na kiwango cha ufaulu shuleni hapo
Ameongeza kuwa, ujenzi huo umewezesha kupatikana kwa chumba cha maktaba ya kuhifadhia vitabu na wanafunzi kujisomea, mara baada ya walimu kuachia chumba hicho kilichokuwa ofisi hapo awali.
"Kiasi hicho cha fedha, kimekamilisha ujenzi wa vyumba 11 vya madarasa, meza na viti 550, kwa kila darasa kuwa na meza na viti 50 pamoja na ofisi mbili za walimu, jambo ambalo limefanya shule hii kuwa na vyumba vya madarasa vya ziada vinavyotumika kwa shughuli nyingine za kielimu". Amesisitiza Mkuu huyo wa shule.
Awali shule ya sekondari Ilkiding'a ni moja ya shule za kata nchini zinazokuwa kwa kasi, ilianza mwaka 1997 ikiwa na wanafunzi 80, kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 1,627 wavulana 733 na wasichana 894.
ARUSHA DC
KaziInaendelea
JIANDAE KUHESABIWA AUGUST 2022.
Mwalimu Tumaini Malkiori, akifundisha wanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Ilkiding'a moja ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa fedha za Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19
Wanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Ilkiding'a wakifurahia kusoma kwenye moja ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa fedha za Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19
Jengo la ghorofa mbili lililojengwa vyumba 10 vya madarasa na ofisi 2 za walimu, shule ya sekondari Ilkiding'a, madarasa yayojengwa kwa fedha za Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.