Na. Elinipa Lupembe.
Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Jamii imetakiwa kutokufumbia macho matukio ya ukatili dhidi ya watoto na kutakiwa kushirikiana na viongozi wa Serikali, kuwafichua watu wahalifu ukatili kwa watoto kwa kutoa taarifa mapema, pindi tu haki ya mtoto inapokiukwa ili kupunguza idadi ya matukio ya ukatili kwa watoto.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha Mhe. Ojung’u Salekwa, wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika halmashauri hiyo, yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya Msingi Sekei.
Mwenyekiti Ojung’u ameweka wazi kuwa, tafiti zinaonesha kuwa, matukio mengi ya ukatili kwa watoto, yanafanyika ndani ya familia zetu na ndugu wa karibu, na jamii inashindwa kuwafichua watuhumiwa hao, kutokana na mahusiano ya undugu katika familia, hivyo ni vema jamii kutambua athari wanazozipata watoto kutokana na matukio hayo, na kuamua kuchukua hatua kama ilivyo makusudio ya serikali.
“Ni wajibu wetu kama viongozi kuwakumbusha wazazi na jamii kutekeleza wajibu wao kwa Watoto, kuwalinda, kuwasikiliza, kuwapa mahitaji yao ya msingi, pamoja na kuwapa taarifa sahihi juu ya ukatili na kuwawezesha kutoa taarifa pindi watakapofanyiwa vitendo hivyo” amesisitiza mhe. Salekwa.
Aidha, Diwani wa Viti Maalum kata ya Kiutu Mh. Nina Masanja amesema kuwa Watoto wote wana haki ya kupata lishe bora, elimu, malazi pamoja na kutobaguliwa na kutoa wito kwa wazazi kuzingatia upendo kwa Watoto wao na kuwapa elimu juu ya vitendo vya kikatili dhidi yao.
“Ukatili wa aina yoyote dhidi ya mtoto haukubaliki kabisa katika jamii yetu, tushirikiane kwa pamoja kutoa taarifa katika vituo Maalum au kupitia namba maalum 116,kwa kufanya hivyo vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vitapungua mpaka kuisha kabisa” amebainisha Mheshimiwa Nina.
Hata hivyo Watoto waliojumuika katika kuadhimisha siku yao muhimu ya Mtoto wa Afrika, wameiomba Serikali kufuatilia kwa ukaribu zaidi ili kubaini matukio ya kikatili yanayofanyika katika jamii inayowazunguka na wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kikatili dhidi ya Watoto wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Arusha, Getruda Darema, ameweka wazi kuwa, halmashauri ya Arusha kwa kushirkina na wadau, inatekeleza mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto kupitia Klabu za watoto shuleni, kamati za MTAKUWWA kuanzia ngazi ya vijiji, pamoja na kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo vijana, wanawake, wazee na viongozi wa dini na mila.
Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika 2022 yenye Kaulimbiu ya “Tuimarishe ulinzi kwa mtoto; Tokomeza ukatili dhidi yake: Jiandae kuhesabiwa”, lengo likiwa ni kuendelea kupambana kupinga ukatili dhidi ya Watoto kwa kuijengea jamii uelewa wa pamoja juu haki za msingi za mtoto.
ARUAHA DC
#KaziInaendelea
JIANDAE KUHESABIWA!!!
PICHA ZA MATUKIO SIKU YA MTOTO WA AFRIKA 2022.
Watoto halmashauri ya Arusha wakiwa na Bango lenye kaulimbiu ya siku ya mtoto wa Afrika 2022, “Tuimarishe ulinzi kwa mtoto; Tokomeza ukatili dhidi yake: Jiandae kuhesabiwa”,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha Mhe. Ojung’u Salekwa, akihutubiwa wananchi wa halmashauri hiyo, wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika, kwenye viwanja vya shule ya Msingi Sekei.
Watoto wa shule ya Msingi Oligilai, wakitoa ujumbe wa siku ya Mtoto wa Afrika, wakati wa maadhimisho ya siku yao maalum kupitia ngoma,kwenye viwanja vya shule ya Msingi Sekei.
Watoto wa shule ya Msingi Green Acress, wakitoa ujumbe wa siku ya Mtoto wa Afrika kupitia wimbo maalum, wakati wa maadhimisho ya siku hiyo,kwenye viwanja vya shule ya Msingi Sekei.
Watoto wa shule ya Msingi Sekei, wakitoa ujumbe wa siku ya Mtoto wa Afrika kupitia igizo maalum, wakati wa maadhimisho ya siku hiyo,kwenye viwanja vya shule ya Msingi Sekei.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.