Na. Elinipa Lupembe.
Jamii imetakiwa kubadili mtazamo na kujenga tabia ya kuzungumza na vijana masuala ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango kuanzia ngazi ya familia, ili kuwawezesha vijana kujitambua na kujiamini katika kukabiliana na mabadiliko ya kawaida ya kimaumbile na tabia zinazotokana na makuzi, na kuweza kuondokana na madhara yanayosababisha ndoa za utotoni na mimba.
Rai hiyo imetolewa na mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arumeru kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Arumeru, mwalimu James Nchembe, wakati wa kufungua warsha ya siku mbili,, iliyomalizika jana na kuwakutanisha vinara wa afya ya uzazi na uzazi wa mpango, kutoka ngazi ya jamii ndani ya halmashauri ya Arusha, iliyofanyika kwenye Kijiji cha kulelea watoto SOS Ngaramtoni.
Katibu Tawala huyo amewataka vinara hao, kwenda kuwa mabalozi wa kuhamasisha na kuelemisha jamii yao, kuwa karibu na vijana na kuwapa elimu ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango, elimu itakayowajengea uwezo wa kutambua mabadiliko ya kimwili, kiakili na kitabia yanayotokana na makuzi, mabadiliko ambayo kimsingi ndio humuweka kijana katika kuandaa maisha yake ya baadaye.
Ameongeza kuwa jamii na wazazi wamekua kimya juu ya elimu hiyo, kwa kuona sio jukumu lao bali ni jukumu la watoa huduma za afya, jambo ambalo si la kweli na linapoteza ndoto za vijana wengi, na kuwasisitia walezi na wazazi kuwa jukumu hilo ni lao, na ni sehemu ya malezi kwa watoto wao.
" Uelewa mdogo wa vijana wengi juu ya afya ya uzazi, ndio unaosababisha mimba za utotoni na ndoa za utotoni, changamoto ambazo zinaua ndoto halisi za vijana wetu, na kuwafanya kukata tamaa na wengine kujiingiza kwenye vitendo viovu" amesema Katibu Tawala huyo
Katibu Tawala huyo, amafafanua kuwa, dhana ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango ina mawanda mapana juu ya kulinda afya, kujikinga na magonjwa ya zinaa, kuweka mipango thabiti ya uzazi sambamba na mipango ya kiuchumi pale kijana anapoamua kuingia kwenye ndoa na si kutumia dawa za uzazi wa mpango pekee kama ilivyo uelewa finyu wa jamii kwa sasa.
Hata hivyo baadhi ya vinara vijana waliohudhuria warsha hiyo, wamethibitisha kuwa, ukimya wa wazazi juu ya afya ya uzazi ni tatizo katika jamii yao, na kuongeza kuwa wao kama vijana, hushindwa kufika hata kwenye vituo vya afya kufahamu afya uzazi na uzazi wa mpango, kutokana na baadhi ya wahudumu wa afya kutokuwakubali na kutoa siri za vijana kwa wazazi au shuleni.
Wameongeza kuwa kikwazo hicho, kinawafanya vijana wengi kushauriana wao kwa wao, matokeo yake hujikuta wamepoteza mwelekeo na wakati mwingine baadhi ya vijana hupoteza maisha, jambo ambalo linaweza kuzuilika kupitia wazazi kwa kushirikiana na wahudumu wa afya katika maeneo ya nyumbani, shuleni na vyuoni pia.
Naye Waziri wa Elimu, serikali ya Wanafunzi Chuo cha Misitu Olmotony, Martine Severine, amethibitisha kuwa, mara nyingi vijana, wameshindwa kuhudhuria kwenye vituo vya afya kufahamu afya ya uzazi na uzazi wa mpango, kutokana na wahudumu wa Afya kuwasiliana na uongozi wa chuo juu matatizo waliyonayo, jambo ambalo linawaacha vijana njia panda na kujikuta wakishauriana wao kwa wao, ushauri ambao hauwapoteza kutokana na ukweli kwamba ushauri huo hukosa taarifa sahihi.
Aidha Vinara hao, wamekubaliana kwenda kuelimisha jamii zao, kuachana na mila potofu za kudhani kumfundisha kijana juu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango ni kumfundisha kuanza tabia za ngono mapema jambo ambalo si kweli bali ni kumuandaa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya kimakuzi.
Naye Muuguzi na Mratibu wa Uzazi wa Mpango, halmashauri ya Arusha, Botolwa Butiku amesema kuwa, halmashauri imejipanga kutumia vinara hao, kufanya mafunzo ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango, kwenye ngazi ya jami ili kuwafikia vijana na watu wa rika zote kwa nje ya vituo vya kutolea huduma za afya.
Amefafanua kuwa, Warsha hiyo ya siku mbili imeandaliwa na halmashauri ya Arusha, kwa kushirikiana na shirika la JHPEIGO kupitia mradi wa Tupange Pamoja 'TCI',iliyowakutanisha Vinara waelimisha rika, kutoka makundi mbalimbali ya jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo vinara hao, kuwa mabalozi wa kuelimisha rika juu ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwenye jamii yao.
Picha ya pamoja ya timu ya vinara walioshiriki kwenye warsha ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Kijiji cha kulelea watoto SOS Ngaramtoni.
Katibu Tawala wilaya ya Arumeru, mwalimu James Nchembe, akizungumza na timu ya vinara wakati akifungua warsha ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Kijiji cha kulelea watoto SOS Ngaramtoni.
Muuguzi na Mratibu wa Afya ya Uzazi na uzazi wa mpango, halmashauri ya Arusha, Botolwa Bujiku akiwasilisha mada kwenye kwa vinara walioshiriki kwenye warsha ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Kijiji cha kulelea watoto SOS Ngaramtoni.
Baadhi ya vinara wakifuatilia mada zilizotolewa kwenye warsha ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Kijiji cha kulelea watoto SOS Ngaramtoni.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.