Na Elinipa Lupembe.
Viongozi wa jamii ya wafugaji yenye asili ya kabila la kimaasai, wametakiwa kuongeza kasi ya kupaza sauti, kwa kuendelea kuelimisha, kuhamasisha jamii zao, kuachana na mila potofu, zinazomkandamiza na kuwakosesha mtoto wa haki za msingi.
Wito huo umetolewa, wakati wa semina ya siku moja ya kuutambulisha mradi mpya wa SAUTI YANGU, iliyowakutanisha wadau mbalimbali kwenye ngazi ya kata wakiwemo, viongozi wawakilishi wa wananchi na viongozi wa serikali, viongozi wa mila na viongozi wa dini, wa kata za Kimnyaki na Mwandet, semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Arusha.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, mkurugenzi wa shirika la Centre for Women and Youth Development (CWCD) Tanzania, Hindu Mbwego, amewataka viongozi hao wa jamii ya wafugaji, kupaza sauti zao kwa kuendelea kuelimisha jamii yao, kubadilika na kuachana na mila potofu, zinazowakandamiza watoto kwa namna moja au nyingine na kuwa na uwajibikaji rafiki kwa watoto utakaowawezesha watoto kuwa huru na wazi mbele ya jamii.
Amewasisitiza kukemea vitendo vinavyofanywa na jamii hiyo kwa kivuli cha mila na desturi na kuvitaja vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto, ni pamoja na watoto wa kike kuchumbiwa wakiwa shuleni, ndoa za utotoni, kukeketa pamoja na ufanyishwaji wa kazi ngumu kwa watoto na kuhakikisha watoto wanapatiwa mahitaji yao ya msingi.
Hindu amefafanua kuwa, mradi wa SAUTI YANGU, unalenga kuhakikisha jamii ina uelewa wa pamoja juu ya haki za mtoto, huku ukiwataka watoto wenyewe kutambua haki zao na kuzisimamia, wakiwa na uwezo wa kutoa taarifa juu ya matukio ya kikatili dhidi yao.
Hata hivyo wadau hao, wamekiri kuwepo kwa vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto na kuthibitisha kuwa vitendo hivyo, hufanywa na jamii yao kutokana na mila na desturi za kabila lao, ambazo kimsingi wamezaliwa na kukuta wazee wao wakizitekeleza na kuongeza kuwa kutokana na elimu wanayoipata, wanaendelea kuelimishana na kuachana na mila hizo.
Diwani wa Kata ya Mwandet, mheshimiwa Boniface Tarakwa, amethibitisha uwepo wa ukatili dhidi ya watoto kwenye kata yake, unaotokana na mila na desturi za kabila lao, ikiwemo ndoa za utotoni na kuongeza kuwa, viongozi wanafanyakazi kubwa kuelimisha jamii yao, na tayari watu wameanza kubadilika, huku akiamini siku zinavyokwenda mila hizo zitakwisha.
"Ni kweli matukio ya ukatili dhidi ya watoto, hasa ndoa za utotoni yapo kwenye jamii yetu, na hii inatokana na mila ambazo tulikuta wazee wetu wanachumbia msichana kuanzia mimba, lakini kwa sasa jamii imeanza kutambua ni udhalilishaji na ni kosa kisheri, wengi wameanza kubadilika" amesema Diwani huyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, mheshimiwa, Noah Lembris, amesema kuwa ukatili dhidi ya watoto, hawezi kwisha kama jamii yenyewe haitakubali kubadilika kimtazamo, kuanzia mtu mmoja mmoja kwenye ngazi ya familia, kwa kuwa haki za watoto wengi zinapotezwa na watu wa ndani ya familia.
"Kesi nyingi za ukatili dhidi ya watoto, zinashindwa kuwapa haki watoto, kutokana na wazazi kukubaliana kumalizana nyumbani na kuacha kuhudhuria mahakamani kutoa ushahidi kwenye kesi hizo.
Wakili wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoa wa Arusha, Mweneti Azael, amesisitiza jamii hiyo kutambua kuwa, haki na Wajibu wao kama wazazi kwa mtoto vinakwenda sambamba, na utekelezaji wake ukienda sawa, ukatili wa mtoto utakuwa umetokomezwa.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Arusha, Getrude Darema, amesema kuwa, mafunzo hayo, yametolewa na halmashauri kwa kushirikiana na shirika la CWCD, kwa lengo la kuwajengea uwezo na maarifa ya ufahamu juu ya haki na ulinzi wa mtoto, ukatili dhidi ya mtoto, kuchambua utendaji wa mfumo wa ulinzi wa mtoto pamoja na kuchukua hatua kwenye vikwazo vya masuala mazima yanayomhusu mtoto.
Awali, Mradi huo wa SAUTI YANGU, unatekelezwa na shirika la CWCD kwa ufadhili wa shirika la Child Fund la nchini Korea, kwenye kata mbili za Mwandet na Kimnyaki.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.