Na Elinipa Lupembe
Halmashauri ya Arusha imeungana na mataifa yote duniani, kuadhimisha wiki ya Unyonyeshaji Dunia, kwa kutoa elimu kwa kina mama na jamii, umuhimu wa unyonyeshaji na lishe bora kwa mama anayenyonyesha kwa kipindi cha miaka miwili.
Elimu hiyo imetolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na mikutano ya jamii, huku jamii ikielimishwa kufahamu umuhimu wa lishe bora kwa mama anayenyonyesha, kutokana na uhitaji mkubwa wa virutubisho mwilini, kwa ajili ya afya yake na kutengeneza maziwa ya mtoto anayemnyonyesha kwa kipindi chote cha kunyonyesha.
Mratibu wa Mama na Mtoto, halmashauri ya Arusha, Butolwa Bujiku, amefafanua kuwa ni muhimu mama anayenyonyesha kula milo kamili zaidi ya mitatu kwa siku na akiongeza asusa katikati ya milo hiyo mitatu.
Bujiku ameongeza kuwa ulaji unaofaa kwa mama anayenyonyesha, humfanya mama kuwa na afya bora na humpatia virutubisho vya kutosha kutokana na ongezeko la mahitaji ya virutubishi wakati wa unyonyeshaji, ambavyo huwezesha mwili wake kutengeneza na kutoa maziwa ya kutosha kadri mtoto anavyohitaji kwa kipindi chote cha miaka miwili.
Aidha lishe bora huimarisha kingamwili ya mama dhidi ya maradhi mbalimbali, kuzuia upungufu wa damu zaidi huongeza akiba ya madini chuma ambayo hutumika kwa mama na kwa mtoto kupitia maziwa ya mama.
"Mama akipata lishe bora kwa kipindi chote cha unyonyeshaji, atakuwa na maziwa yakutosha, yanayomuwezesha mtoto kuwa na afya bora na kukua vizuri kimwili, kiakili na kisaikolijia na zaidi maziwa ya mama huimarisha kinga ya mama na mtoto dhidi ya magonjwa na kujenga akili ya mtoto.
Naye Afisa Lishe halmashauri ya Arusha Doto Milembe, ametaja mlo kamili unatakiwa angalau kuwa na mchanganyiko chakula kimoja kutoka makundi matano ya vyakula ikiwemo wanga na mizizi, nyama, mafuta, mbogamboga, matunda, virutubisho vyenye madini ya chuma, maji na chumvi yenye madini joto.
Ameongeza kuwa ulaji wa vyakula vyenye asili ya wanyama kama nyama, kuku, mayai, maziwa, samaki, dagaa vina virutubisho kwa wingi ikiwemo protini na madini chuma ambayo husaidia kuongeza damu mwilini, na kusisitiza ulaji wa matunda ya aina mbali mbali na mbogamboga kwa wingi una vitamini kwa wingi ambazo huongeza kinga mwilini.
Afisa Lishe huyo amesisistiza mama anayenyonyesha kunywa maji ya kutosha angalau Lita moja na nusu kwa siku, pamoja na kumeza vidonge vya kuongeza damu (FEFO) kwa kipindi cha miezi 3 baada ya kujifungua.
Hata hivyo Kaimu Mganga Mkuu, Halmashauri ya Arusha Dkt. Japhet Champanda, amebainisha kuwa mama anayenyonyesha licha ya kupata lishe bora anatakiwa kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kama vile malaria kwa kulala kwenye chandarua kilichowekwa dawa na kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na virusi vya UKIMWI.
Dkt. Champanda amesisitiza kuwa, ni muhimu mama anayenyonyesha kusaidiwa kazi nzito ili apate muda wa kutosha wa kupumzika na kumnyonyesha mtoto mara kwa mara kila anapohitaji, usiku na mchana.
Awali kilele cha maadhimisho ya Wiki ya unyonyeshaji kitaifa yatafanyika mkoani Singida yakiwa na Kauli Mbiu ya "Chukua hatua endeleza unyonyeshaji: Elimisha na toa Msaada".
SHIRIKI SENSA YAWATU NA MAKAZI 2022.
JIANDAE KUHESABIWA 23.08.2022
Muuguzi kituo cha Afya Oldonyosambu akimuelekeza mama namna ya kumnyonyesha mtoto, ikiwa ni shughuli za Maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshajio Duniani katika Halamshauri ya Arusha.
Muuguzi Kituo cha Afya Oldonyosambu Vaileth Chahe, akitoa Mafunzo ya umuhimu wa unyonyeshaji na lishe bora kwa mama na mtoto, ikiwa ni shughuli za Maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshajio Duniani, halmasahuri ya Arusha.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.