Na. Elinipa Lupembe.
Jumuia ya wanafunzi waliosoma shule ya sekondari Oldonyosambu (OSESA) wametoa msaada wa mashine ya kudurufu karatasi (photocopy machine) yenye tahamani ya shilingi milioni 3, kwa shule ya sekondari Oldonyosambu, ikiwa ni ishara ya kurudisha fadhila kwenye shule waliyosoma.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi hao na mjumbe wa OSESA, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Paulo Losule, amesema kuwa, umoja huo wa wanafunzi waliosoma shuleni hapo miaka ya nyuma, umeguswa na juhudi zinazofanywa na serikali na shule hiyo kitaaluma na kuamua kutoa mashine hiyo ili itumike kudurufu mitihani, mitihani ambayo wanaamini, itawajengea uwezo na kujiamini wanafunzi, jambo litakalowezesha kupanda kwa ufaulu shuleni hapo.
Dkt. Losule ameweka wazi kuwa, wakati wakisoma hapo, shule haikuwa na miundombinu mingi na mizuri kama sasa, haikuwa na walimu wa kutosha, lakini kwa sasa serikali imewekeza sana katika shule hiyo, na kuwatia moyo wanafunzi licha ya kuwa wanatokea kwenye mazingira magumu, wasikatishwe tamaa na hilo, badala yake kufanya bidii kwenye masomo, ili kufaulu na kufikia malengo yao ya baadaye.
"Elimu ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani, msidanganyike kwamba hata bila kusoma maisha yanawezekana, tambueni bila elimu changamoto ni nyingi sana, kuna tofauti kubwa kati ya mtu mwenye elimu na asiye na elimu, wadogo zangu mmepata fursa hii, tumieni kwa kusoma kwa bidii".Amesisitiza Dkt. Losule
Naye mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, licha ya kuishukuru jumuia ya ASESA, ameipongeza pia kwa maono makubwa waliyonayo kwa jamii yao, hasa kwa kukumbuka walikotoka, jambo ambalo wengi hawalifanyi.
Aidha Mkurugenzi Msumi, ameupongeza uongozi wa shule ya sekondari Oldonyosambu, walimu, wanafunzi na wazazi kwa kuwa na juhudi za kupandisha taaluma ya shule hiyo, bidii ambazo zinavutia wadau kuchangia maendeleo ya shule hiyo kama ilivyo kwa OSESA.
Awali, Diwani wa kata ya Oldonyosambu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii, Mheshimiwa Raymond Lairumbe, amewataka wazazi kutimiza wajibu wao kwa kutekeleza majukumu yao, hasa katika kuwahudumia watoto wao wawapo shuleni, na kuweka wazi kuwa, tayari wanaona matunda ya shule hiyo kupitia jumuia ya OSESA.
"Tunashuhudia matunda ya Oldonyosambu, shule imezalisha watalam wa fani mbalimbali, na wametawanyika Tanzania nzima, wazazi timizeni wajibu wenu, simamieni watoto wenu kusoma bila kuwakatisha masomo yao, ili nao waje kuwa madaktari, walimu, wahasibu, wahandisi na watalamu katika nchi hii, jamani hili linawezekana na sio miujiza". Amesisitiza Mheshimiwa Diwani huyo.
Naye Mkuu wa shule ya Oldonyosambu, mwalimu Leshai Moita, ameishukuru ASESA kwa kuendelea kupambania maendeleo ya ndugu zao, na shule kwa ujumla, na kuwaahidi kuwafundisha kwa bidii wanafunzi waliopo, ili nao waweze kutimiza ndoto zao pamoja na kuwaandaa kuwa wana OSESA wa baadaye, wenye maono makubwa zaidi.
Hata hivyo katika hafla hiyo, Bank ya TIB nayo ilikabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi bati na mbao, vifaa kwa ajili ya kupaua jengo la utawala la shule hiyo, vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 3.
Shule ya sekondari Oldonyosambu ni shule ya kata, ilianza mwaka 1996, ni shule inayoendelea kukua kwa kasi kitaaluma, kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2021, imeshika nafasi ya pili katika halmashauri ya Arusha ikiifuatia nyuma shule ya Maalum ya sekondari Ilboru.
ARUSHA DC
KaziInaendelea✍
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi akipokea mashine ya kudufu karatasi, kutoka kwa mwakilishi wa Jumuia ya wanafunzi waliosoma shule ya sekondari ya Oldonyosambu ( ASESA) Dkt. Paulo Losule (wa kwanza kulia), mashine iliyotolewa kwa ajli ya matumizi ya shule ya sekondari Oldonyosambu.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi (kulia) akipokea mabati, kutoka kwa Meneja wa TIB Bank tawi la Arusha (jina halikupatikana), mabati yayotolewa kwa ajli ya kupaulia jengo la Utawala shule ya sekondari Oldonyosambu.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi (kulia) akipokea mbao, kutoka kwa Meneja wa TIB Bank tawi la Arusha (jina halikupatikana), mbao zilizotolewa kwa ajli ya kupaulia jengo la Utawala shule ya sekondari Oldonyosambu.
Mwakilishi wa Jumuia ya wanafunzi waliosoma shule ya sekondari ya Oldonyosambu ( ASESA) Dkt. Paulo Losule, akizungumza na jumuia ya Oldonyosambu sekondari wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mashine iliyotolewa na jumuia hiyo, kwa ajli ya matumizi ya shule ya sekondari Oldonyosambu.
Afisa Elimu sekondari, halmashauri ya Arusha, Mwalimu Menard Lupenza, akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano wa masaada wa Mashine ya Kudurufu iliyotolewa na jumuia ya wanafunzi waliosoma shule Oldonyosambu (ASESA).
Jengo la Utawala sekondari Oldonyosambu, TIB Bank wametoa msaada wa mabati na mbao kwa ajili ya kukamilisha upauzi wa jengo hio.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.