Na. Elinipa Lupembe.
Kamati ya kudumu Bunge ya kilimo, mifugo na maji imeipongeza Halmashauri ya Arusha, kwa juhudi kubwa zilizofanyika katika utekelezaji wa mirafi ya maji ya vijiji kumi iliyokuwa ikifadhiliwa na Benki ya Dunia, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo katika halmashauri hiyo.
Kamati hiyo imetembelea mradi wa maji wa Loovilukuny uliokamilika kwa asilimia 95% na mradi wa maji wa Ngaramtoni uliokamilika kwa asilimia 100% iliyogharimu kiasi cha shilingi Bilion 1.4 mpaka sasa.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa, Mahammud Mgimwa, amesema kuwa, halmashauri ya Arusha ni moja ya halmashauri iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maji ya vijiji kumi, juhudi zilizowezesha, mafanikio makubwa katika miradi ya maji.
Mwenyekiti huyo, amezitaka halmashauri nyingine hapa nchini, zinazotekeleza miradi hiyo ya maji kuiga mfano wa halmashauri ya Arusha, kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa kufuata taratibu zilizopo.
"Halmashauri ya Arusha ni miongoni mwa halmashauri chache zilizotekeleza miradi ya maji ya vijiji kumi, kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na Halmashauri zingine hapa nchini, halmashauri nyingine hazibudi kuiga utendaji kazi wa halmashauri hii" amesema Mh Mgimwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amesema kuwa, kwasasa wananchi wa halmashauri ya Arusha wanapata maji safi, kwa asilimia 57.9% na wanatarajia kufikia asilimia 61.67% pindi miradi yote iliyosalia itakapokamilika.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha Dk. Wilson Mahera amebainisha siri kubwa ya mafanikio, katika utekelezaji wa miradi hiyo, ni pamoja na usimamizi makini wa siku hadi siku, usimamizi wa matumizi sahihi ya pesa, kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.
"Tumekuwa na usimamizi wa karibu wa utekelezaji wa miradi na matumizi ya fedha pamoja na kuwatumia wadau mbalimbali, wataalamu pamoja na wananchi kwa kuwaweka pamoja katika kutekeleza miradi hii na ndio sababu tumefikia hapa" amesema Dk. Mahera
Nao wananchi wa Ngaramtoni, hawakuwa nyuma kuishukuru serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa usimamizi thabiti wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha zaidi wananchi wa hali ya chini ambao ndio wahitaji zaidi.
John Mollel mkazi wa Ngaramtoni amesema kuwa, tunaishukuru sana serikali ya awamu ya tano, serikali ambayo imejikita kwenye kuwahudumia wananchi wa hali ya chini na kuongeza kuwa miradi hiyo ya maji imewanufaisha wanchi ambao walikuwa wakiteseka na upatikanaji wa majibyasiyo ya uhakika kwa kipindi kirefu.
Awali jumla ya miradi minne kati ya kumi imekamilika, ikiwemo mradi wa maji Ilkirevi, na Oloigueruno, Nduruma, Loovilukuny na Ngaramtoni, na tayari wananchi wameanza kupata maji, huku miradi mingine sita iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na inategemea kukamilika kabla ya mwaka ujao wa 2020.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.