Na.Elinipa Lupembe.
Klabu ya Rotary inayoundwa na wananchi wa kijiji cha Landsbay cha nchini Denmark kwa kushirikiana na Klabu ya Rotary ya Njiro jijini Arusha, imeendelea kuboresha miundo mbinu ya shule ya sekondari Oldonyowas, halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, tangu kuanzishwa kwa ujenzi wa shule hiyo mpya mwaka 2017, baada ya kukabidhi vyumba viwili vya madarsa na maabara ya somo la Kemia na Baiolojia kwa serikali.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano na uzinduzi wa majengo hayo mawili,kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Arumeru, Eng. Richard Ruyango, mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha Selemani Msumi, amewashukuru wananchi wa Denmark wanaounda klabu hiyo, kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita, kuboresha miundombinu ya elimu, na kuhakikisha watoto wa kitanzania wanasoma katika mazingira bora na salama.
Hata hivyo mkurugenzi Msumi, licha ya kupongeza juhudi za Klabu hiy, amewataka walimu na wanafunzi kutambua thamani ya majengo hayo, kwa kuyatunza na kuongeza bidii katika kupandisha kiwango cha taaluma shuleni hapo, huku akiwasisitiza wanafunziwa shule hiyo, kusoma kwa bidii, kwa kuwa tayari serikali imesimami uwepo wa mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia.
"Jukumu lenu wanafunzi kwa sasa ni kuhakikisha mnasoma kwa bidii, na kufaulu vizuri katika masomo yenu, kwa kuwa tayari mazingira ya kujifunzia ni rafiki, wekeni nidhamu mbele 'be ethical, do right thing' fuata maadili tenda kwa usahihi, lakini pia onyesheni juhudi ili kuwatia moyo, wananchi wa Denmark waweze kuendela kuwasaidia, wananchi wa Denmark wamejitoa kwa moyo, msiwakatishe tamaa" amesisitiza Mkurugenzi Msumi
Naye mwakilishi wananchi wa kijiji cha Lasbay nchini Denmark, Jespa Gregersen, amesema kuwa Klabu hiyo imefanikisha kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na samani zake kwa gharama ya shilingi milioni 54, huku jengo la maabara na miundombinu yake likighatimu kiasi cha shilingi milioni 64, majengo ambayo yamekamilika na yamezinduliwa na kukabidhiwa kwa serikali, tayari kwa kutumiwa na wanafunzi wa Oldonyowas.
Amefafanua kuwa lengo la ujenzi wa miundombinu hiyo shuleni hapo, ni kuwawezesha wanafunzi kupata elimu katika mazingira bora, na kuahidi kuwa hivi karibuni klabu hiyo inakusudia kuanza ujenzi wa bwalo la chakula na jiko, lengo likiwa kuwawezesha wanafunzi kupata chakula kwenye mazingira rafiki pia, kwa kuwa elimu bora inaenda sambamba na afya bora.
"Ninawashukuru wananchi wa kijiji cha Oldonyowas kwa kunipa ushirikiano mkubwa, katika kila hatua ya maendeleo tunayopanga pamoja, tunakufikia malengo kwa wakati, ninaamini ujenzi wa majengo hayo yote, umewezekana kutokana na wananchi wa kijiji hiki, kuwa na kiu sana ya maendeleo" amesisitiza Jespa mdau huyo wa maendeleo.
Hata hivyo mwenyekiti wa kijiji cha Oldonyowas Mheshimiwa Geophray Ayo, licha kuishukuru klabu hiyo ya Rotary kupitia Bwana Jespa, amemuomba kutokuchoka kuendelea kuisaidi shule hiyo mpya, kwa kuwa bado inakabiliwa na upungufu wa baadhi ya miundombinu muhimu ikiwemo Maktaba pamoja na bweni la wanafunzi kiume, watoto ambao hutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule kila siku, jambo ambalo linakatisha tamaa kwa baadhi ya wanafunzi kuendelea na shule.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa shule ya sekondari Oldonyowas, Rais wa serikali ya wanafunzi Mika Ismail (kidato cha III), ameishukuru klabu hiyo ya Rotary kwa misaada wanayoitoa kwa shule yao, na kuahidi kuyatunza majengo hayo, pamoja na kuhimiza wanafunzi wote kuongeza bidii katika masomo yao ili kupandisha kiwango cha taaluma na ufaulu wa shule hiyo katika matokeo ya mitihani ya ndani na ile ya kitaifa.
Klabu hiyo ya Rotary ya nchini Denmark imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika kijiji cha Oldonyowas tangu mwaka 1992 na imefanikiwa kuwekeza miradi katika seka ya elimu, afya na maji, kwa kujenga mradi wa maji, zahanati pamoja na kushiriki bega kwa bega katika mipango ya uanzishwaji wa ujenzi wa shule hiyo ya sekondari ya Oldonyowas.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, anaendelea kuwakaribisha wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi, kusaidia kuboresha miundombinu ya shule za sekondari na msingi katika halmasahauri ya Arusha.
HABARI KATIKA PICHA
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Selemani Msumi (kushoto) na Mwakilishi wa Rotary Klabu ya Denmark, Jespa Gregersen, wakizindua jengo la vyumba viwili vya madarasa, shule ya sekondari Oldonyowas, wakati wa hafla ya kukabidhi majengo hayo kwa serikali.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi akiwa ndani ya darasa jipya, shule ya sekondari Oldonyowasi, mara baada ya kuzinduliwa na kukabidhiwa jengo hilo na mwakilishi wa Klabu ya Rotary inayoundwa na wananchi wa kijiji cha Landsbay cha nchini Denmark bwana Jespa Gregersen (hayupo pichani).
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Selemani Msumi (kushoto) na Mwakilishi wa Rotary Klabu ya Denmark, Jespa Gregersen, wakizindua jengo la Maabara ya Kemia & Baiolojia, shule ya sekondari Oldonyowas, wakati wa hafla ya kukabidhi majengo hayo kwa serikali
Wanafunzi wa kidato cha tatu, shule ya sekondari Oldonyowas, Linda Mgimba (wa kwanza kulia) na Venancia Metishili wakielezea matumizi ya vifaa vya maabara na namna ya kuchanganya kemikali mbalimbali kwa kutumia vifaa hivyo vya maabara, mara baada ya jengo la maabara hiyo kuzinduliwa.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.