Mwanzilishi wa mradi wa maji wa vijiji vitano maarufu kama mradi wa WaterAid, halmashauri ya Arusha na mkurugenzi wa shirika lilisilo la kiserilalo la TUMAINI JIPYA-NEW HOPE, Louise Richardson, amewasili nchini na kukutana na viongozi wa serikali, wananchi pamoja na kutembelea maeneo mbalimbali kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa maji.
Louise Richardson, raia wa Uingereza na Diwani wa Kaunti ya Leicestershine Jimbo la Blaby nchini Uingereza ndiye 'founder' wa mradi wa maji wa vijiji vitano baada ya kuishi kwa muda kama 'volunteer' katika kijiji cha Lengijave kata ya Olkokola, halmashauri ya Arusha.
Katika kuishi kwake Lengijave na kushuhudia adha kubwa ya maji inayowakabili wakazi wa Lengijave na maeneo ya jirani, Diwani Louise aliguswa na kuamua kwenda nchini kwake Uingereza, kutafuta fedha ili wananchi hao wapate huduma ya maji na kuondokana na adha hiyo.
Hata hivyo serikali ya Uingereza kupitia Idara yake ya Maendeleo ya kimataifa 'DFID' imefadhili utekelezaji wa mradi wa maji kwa vijiji vitano vya Lengijave, Olkokola na vitongoji vya Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni, mradi utakaogharimu shilingi bilioni 4.5.
Mradi huo kwa sasa uko katika hatua ya uchimbaji visima, usanifu na upembuzi yakinifu wa miundombinu ya maji na unategemea kukamilika mwezi Septemba mwaka huu wa 2018.
Katika ziara yake, Diwani Louise amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi na timu ya watalamu wa mradi wa maji halmashauri ya Arusha, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha na timu ya watalamu wa mradi ya mkoa, viongozi na baadhi ya wananchi wa kata, katika eneo la mradi pamoja na timu ya usanifu wa mradi wakiwa kazini.
Aidha Louise ametembelea eneo la shamba la Kilimo, mahali kulipochimbwa visima viwili kwa ajili ya mradi huo nakujionea visima vikiwa tayari vimechimbwa.
Hata hivyo Louise ameonesha kuridhishwa na hatua zilizofikiwa za maendeleo ya utekelezaji wa mradi pamoja na ushirikishwaji wa wananchi kuhusu mradi huo, unaoleta uelewa wa pamoja kuhusu mradi.
Diwani Louise amefurahishwa zaidi na kauli za wanainchi aliofanikiwa kukutana nao katika maeneo ya mradi, za kuonesha kuufahamu vema mradi licha ya kuwa bado uko kwenye hatua za utekelezaji pamoja na ushirikiano wanaoutoa kwa watalamu watekelezaji wa mradi.
Wananchi na viongozi wamepata fursa ya kumuelezea Diwani Louise kuwa, kutokana na shida ya maji inayowakabili kwa kipindi kirefu sasa, jamii imepokea mradi kwa mikono miwili na inatoa ushirikiano mkubwa kwa watalamu wanaofika kwenye maeneo yao katika hatua zote kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji.
Baadhi ya wananchi wamekuwa na wasiwasi kwa kuona kama mradi unachelewa kukamilika, hadi kufikia wakati mwingine kuingia kwenye maombi,kumuomba Mungu mradi ukamilike haraka.
Hata hivyo Louise amewashauri watalamu wa usanifu kuwa waangalifu kwenye maeneo ya kupitisha miundombinu ya maji kwa kukwepa kupitisha kwenye alama za kudumu kama makaburi, kukwepa kubomoa nyumba za watu ili kusiwe na migogoro itakayoweza kukwamisha mradi kukamilika kwa wakati pamoja na kuepuka gharama zinazoweza kuongezeka kwa ajili ya fidia.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.