Na. Elinipa Lupembe.
Madiwani wa halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru wametakiwa kutoa elimu kwa jamii wanayoiongoza, juu ya Afya ya Uzazi na Uzazi wa mpango ili kupunguza vifo vya mama na mtoto katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa mradi wa ‘Tupange Pamoja – The Challenge Initiative’ unaotekelezwa na Shirika la Kimataifa la JHPIEGO, uzinduzi ulioambatana na semina elekezi kwa waheshimiwa madiwani wa kata 27 za halmashauri ya Arusha, semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Afisa Tarafa ya Moshono, Tatu Furahisha, amewataka madiwani hao kushiriki kikamilifu kuelimisha wananchi katika maeneo yao, juu ya Afya ya Uzazi na Uzazi wa Mpango, ili kupunguza na kumaliza kabisa vifo vya mama na mtoto katika halmashauri ya Arusha.
Aidha Afisa Tarafa huyo, amewasihi waheshimiwa madiwani hao, afya ya uzazi na uzazi wa mpango kuifanya kuwa agenda ya kudumu, katika vikao vyao na kuongeza kuwa, suala la afya ya binadamu halihitaji siasa, kama viongozi wa wananchi, kupitia mafunzo haya, watumie majukwaa yao, pindi wanapokutana na wananchi kuelimisha wananchi juu ya jambo hilo muhimu.
Bi. Tatu amefafanua kuwa, ripoti ya mwaka 2018, inaonyesha asilimia kubwa ya vifo vya mama na mtoto katika halmashauri ya Arusha, vinatokana na ucheleweshwaji wa wajawazito, kufika hospitali mara wanapopata uchungu wa kujifungua, kwakushirikiana kwa pamoja, tatizo hili litakwisha kabisa, kwa kuwa vifo hivyo sio vya lazima na vinaweza kuepukika.
“Tumieni majukwaa yenu, kwenye vikao vya kata (WDC), mikutano ya vijiji, vikao vya ukoo na mila pamoja na mazungumzo ndani ya familia, kuelimisha jamii umuhimu wa afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na kuhudhuria kliniki muda wote, pindi mama anapogundua ni mjamzito, pamoja na kujifungulia kwenye vituo vya afya na si kujifungulia nyumba” amesisisti Bi. Tatu
Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, Halmashauri ya Arusha, Butolwa Bujiku, amesema kuwa, pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na serikali juu ya uzazi salama, lakini bado kuna changamoto ya mila na desturi za jamii ya kimasai, ambayo wajawazito bado wanajifungulia nyumbani, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.
Ameongeza kuwa, asilimia kubwa ya vifo vya mama na mtoto vilivyotokea mwaka 2018, vimesababishwa na wajawazito kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya, tatizo ambalo linaweza kuepukika kama jamii itakubali kuelimika na kubadilika kwa kuachana na mila hizo potofu.
Aidha mratibu Butolwa, amewataka kina baba kufanya maandalizi mapema ya mama mjazito kujifungua, hasa kwa kuzingatia tarehe za matarajio, kwa kuandaa usafiri wa kumpeleka mama huyo hospitali, pindi anapoanza kupata dalili za uchungu, na kuwataka kuacha tabia ya kuwachelewesha kufika hospitali.
“Wajawazito wengi wakifikia kwenye uchungu wanakaa na kokoo (bibi), mpaka hali ikiwashinda ndio humleta mgonjwa hospitali huku akiwa tayari amechelewa na matokeo yake mtoto au mama, au wote kupoteza maisha, ndugu zangu afya ya mtu haijaribiwi, wawaisheni wajawazito hospitali” amesistiza Butolwa
Mratibu wa Shirika la kimataifa la JHPIEGO mkoa wa Arusha, Waziri Njau amesema kuwa, kupitia mradi wa ‘Tupange Pamoja', ambao umezinduliwa katika halmashauri ya Arusha, utawezesha wananchi kujiongezea maarifa,ujuzi, mbinu na uelewa zaidi juu ya Afya ya Uzazi na uzazi wa mpango, kwa kutumia njia salama, ambazo kimsingi zitaondoa vifo visivyo vya lazima vya mama na mtoto.
Hata hivyo, waheshimiwa madiwani hao, wameridhishwa na mafunzo hayo na kuthibitisha kuwa, yamewaongezea uelewa na maarifa zaidi juu ya Afya ya Uzazi na Uzazi wa mpango huku wengine wakikiri kuwa, awali walifahamu uzazi wa mpango ni kuzuia kuzaa watoto wengi, na kumbe kuna mengi zaidi ya kiafya juu ya uzazi wa mpango na afya ya uzazi pamoja na afya ya familia kwa ujumla.
Diwani wa kata ya Mlangarini, Mheshimiwa Godfray Mashele, amesema kuwa kupitia semina hiyo elekezi, ameweza kupata maarifa zaidi juu ya Afya ya uzazi wa Mpango pamoja na umuhimu wa mama mjamzito kujifungulia hospitali, huku akikiri kuwa watu wengi, ndani ya jamii yake hutumia njia za asili za uzazi wa mpango, njia ambazo amegundua si salama kiafya.
Aidha, Mheshimiwa Mashele amewataka viongozi wenzake, kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, viongozi wa koo na mila kuungana na serikali, kupiga vita wajawazito kujifungulia nyumbani, kwani ni hatari na husababisha vifo vya mama na mtoto na badala yake kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa afya uzazi na uzazi wa mpango,ambayo ni njia salama kwa watoto na wajawazito.
Awali, Shirika hilo la Kimataifa la JHPIEGO limetoa kiasi cha shilingi milioni 181 kupitia udhamini wa mfuko wa 'Bill and Melinda Gate Foundation', kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Afya ya Uzazi na Uzazi wa Mpango na Afya Vijana, katika halmashauri ya Arusha, mradi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia 2019/2020 mpaka 2020/2021, huku halmashauri ya Arusha ikitenga kiasi cha shilingi milioni 32, kwa lengo la kupunguza na kumaliza kabisa vifo vya mama na mtoto wakati wa ujauzito na siku arobaini baada ya kujifungu.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.