Na. Elinipa Lupembe.
Jamii imetakiwa kuelewa kuwa, kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo bila kumpa chakula kingine, huimarisha kinga ya mwili, inayomkinga dhidi ya maradhi pamoja na kumjenga mtoto kiakili na kisaikolojia.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Afya ya Uzazi, na muuguzi hospitali ya wilaya Olturumet, halmashauri ya Arusha, Butolwa Bujiku, wakati akitoa elimu ya unyonyeshaji kwa viongozi na wakazi wa kijiji cha Oltulelei kata ya Ilboru, katika shughuli za kuadhimisha ya wiki ya Unyonyeshaji Duniani 2020.
Butolwa ameeleza kuwa, mama baada ya kujifungua, anatakiwa kumnyonyesha mtoto, kwa kipandi cha miezi sita ya mwanzo bila kumpa chakula kingine chochote, jambo ambalo linajenga afya ya mtoto, ikiwa ni pamoja na kumjengea kinga ya mwili dhidi ya maradhi, kujenga mtoto kiakili na kisaikolojia pia.
Amewataka wazazi kuacha tabia ya kumpa mtoto chakula kingine chochote, kwa kuwa maziwa ya mama yana lishe na virutubisho vya kutosha kwa miezi sita ya mwanzo na kuongeza kuwa, kuanza kumpa mtoto chakula kwa kipindi hicho, huharibu mfumo mzima wa ukuaji wa mtoto, na madhara yake huonekana katika kipindi chote cha maisha yake.
"Kuanza kumpa mtoto chakula kabla ya kufikisha miezi sita, kuna madhara makubwa kwa mtoto, huaribu mfumo wa mzima wa ukuaji wa mtoto, huchosha utumbo na mfumo wa mmeng'enyo, huleta udumavu wa mwili na akili na humuathiri mtoto kisaikolojia, ni vema kuzingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ili kuepuka madhara hayo kwa mtoto" amesisitiza Mratibu huyo.
Naye Afisa Lishe Halmashauri ya Arusha, Doto Milembe amewaondoa wasiwasi watu wanadhani maziwa ya mama peke yake, hayatoshi kwa lishe ya mtoto na kusisitiza kuwa, maziwa yhayo yana virutubisho vya kutosha kwa mtoto wa chini ya miezi sita, yakiwa na viini lishe vya makundi yote ya vyakula pamoja na maji.
Aidha ameitaka jamii kufahamu kuwa, jukumu la unyonyeshaji mtoto si la mama peke yake bali ni jukumu la familia na jamii kwa ujumla ili kuwa na kizazi chenye afya bora kwa maendeleo ya familia, jamii na Taifa.
Hata hivyo viongozi wa kijiji cha Oltulelei, wamekiri kuridhishwa na mafunzo hayo, kwani yamewapa uelewa mkubwa juu ya umuhimu wa kumnyonyeshaji mtoto kwa miezi sita ya mwanzo, jambo ambalo hapo awali hawakufahamu umuhimu wake kwa kina na kuomba elimu hiyo itolewe kwa jamii nzima ili kuwa na watoto wenye afya bora kwa maendeleo ya Taifa lao.
"Tumerishwa na mafunzo haya, yametuondoa gizani kwani wengi tulidhani haiwezekani maziwa ya mama kumtosheleza mtoto, kumbe maziwa ya mama yanatosha na yana virutubisho vyote katika makundi yote ya vyakula" wamesema viongozi hao.
Tatu Shabani mkazi wa kitongoji cha Oltulele amekiri kuwa, licha ya kuwa yeye ni mama mwenye watoto lakini hakufahamu sana, madhara yanayotokana na kuanza kumpa mtoto chakula kabla ya kufikisha miezi sita, na kukiri kuanza kutumia maarifa hayo na kuendelea kuitoa elimu hiyo kwa watu wanomzunguka.
Halmashauri ya Arusha, imeungana na mataifa mengine duniani, kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji Duniani 2020, kwa kutoa elimu na kuhamasisha jamii umuhimu wa mama kunyonyesha mtoto kwa miezi sita ya mwanzo bila kumpa kitu chochote na kumnyonyesha kwa siku 1000.
"Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji Duniani 2020, yamebeba Kauli Mbiu ya Sote kwa pamoja: Tuwawezeshe wanawake Kunyonyesha kwa Afya Bora na Utunzaji wa Mazingira"
Mratibu wa Afya ya Uzazi halmashauri ya Arusha, Butolwa Bujiku akitoa elimu ya unyonyshaji kwa viongozi wa Kitongoji cha Oltulele kata ya Ilboro ikiwa ni Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji, halmashauri ya Arusha.
Viongozi wa Kitongoji cha Oltulele kata ya Iboru wakifuatilia mijadala ya elimu ya unyonyeshaji.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.