Na Elinipa Lupembe
Serikali ya awamu ya sita, licha ya kuwa na mpango wa kuboresha miundombinu ya shule, mpango huo unaenda sambamba na ujenzi wa nyumba za walimu, lengo likiwa ni kurahisisha tendo la kujifunza kwa mwananfunzi na kufundisha kwa walimu.
Katika utekelezaji wa mpango huo, halmashauri ya Arusha imepokea kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 4 za walimu wa shule 4 za msingi katika halmashauri hiyo, wilaya ya Arumeru.
Akizungumza na mwandishi wetu, ofisini kwake Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amebainisha kuwa kiasi hicho cha fedha kinakwenda kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 4 za walimu kwa shilingi milioni 50 kwa kila nyumba.
Aidha ameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuelekeza fedha hizo kujenga nyumba za walimu kwa shule za pembezoni mwa mji, shule ambazo katika maeneo hayo walimu hulazimika kuishi mbali na shul kwa kukosekana kwa nyumba za kupanga karibu na shule.
"Fedha hizi zimeelekezwa kujenga nyumba za walimu shule ya msingi Ereto kata ya Laroi, Shule ya Msingi shikizi Engedeko kata ya Oldonyowas, shule ya msingi Olokii - Shikizi Olmapinuu kata ya Bwawani na shule ya msingi Olemedeye kata ya Nduruma, shule zote ziko umbali wa kati ya Kilomita 40 na 60 kutoa makao makuu ya halmashauri" Ameweka wazi Mkurugenzi huyo
Hata hivyo walimu wanaofundisha shule hizo, licha ya kuishukuru serikali kwa ujenzi wa nyumba za walimu katika shule zao, wamebainisha changamoto kubwa inayowakabili walimu ya mahali pa kuishi, kutokana na kutokuwepo kwa nyumba za kupanga katika vijiji hivyo.
Wamefafanua kuwa walimu wanalazimika kuishi mjini kati ya Kilomita 40 - 60 kutoka shuleni, kutokana na wenyeji wa maeneo hayo kutokuwa na desturi ya kujenga nyumba za kupangisha, lakini ujenzi wa nyumba hizo shuleni utatuwezesha walimu kufanyakazi kwa utulivu kwa kuishi ndani ya eneo la shule.
Mwalimu mkuu shule ya msingi Engedeko, Mwl. Gideon Sombe, ameipongeza serikali pia kwa kuwa, shule hiyo ni mpya imeanza mwaka huu 2022, baada ya serikali kujenga vyumba 4 vya madarasa kwa fedha za UVIKO 19 na kufafanua kuwa ujenzi wa nyumba ya mwalimu, utaboresha hali ya taaluma shuleni hapo.
"Shule ya Engedeko ilikuwa ni shule shikizi, baada ya madara 4 ya UVIKO 19, imesajiliwa na kuwa shule ya Msingi, na ina walimu wanne na haina nyumba hata moja, hivyo ujenzi wa nyumba hii, itakuwa ni miongoni mwa shule zinazokuwa kwa kasi, na kukidhi mahitaji ya walimu na elimu kwa watoto wa kijiji cha Losinoni Juu". Amefafanua Mwalimu Sombe
Wananchi wa Halmashauri ya Arusha, kupitia uongozi wa halmashauri hiyo, unaipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
ARUSHA DC
KaziInaendelea ✍ ✍
RAMANI YA NYUMBA HIZO
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.