Na Elinipa Lupembe
Mkulima Isaya Lomayani kutoka Kata ya Mwadent, halmashauri ya Arusha, amekuwa mkulima bora kwa kushika nafasi ya kwanza kwa mkoa wa Arusha, kwenye maonesho ya Nanenane kanda ya Kaskazini yanayofanyika kwenye viwanja vya nanenane eneo la Themi -Njiro Jijini Arusha.
Isaya Lomayani amekabidhiwa kombe kubwa na Mgeni rasmi wakati wa kufunga maonesho hayo, mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere, mara baada ya kuwabwaga wakulima kutoka halmasahuri zote saba za mkoa wa Arusha
Mkulima Lomayani anayejihusisha zaidi na kilimo cha mboga mboga na mahindi, amekiri kilimo hicho kumuingizia kipato kutokana na kufuatilia maelekezo anayopatiwa na watalamu wa halmashauri ya Arusha sambamba na kumuunganisha na wadau na makampuni yanayojihusisha na mbegu bora na masoko.
"Ninalima mbogamboa na mahindi, kilimo ambacho nimekiboresha miaka ya hivi karibuni na kukifanya kilimo biashara, mara baada ya kupata mafunzo ya teknolojia ya uzalishaji bora kutoka kwa mtalamu wa kilimo kwenye kata yangu ya Mwandet kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo" Amefafanua Lomayani
Lomayani licha ya kuushukuru uongozi wa mkoa wa Arusha na waandaaji wa Maonesho hayo, ameweka wazi kuwa maonyesho ya nanenane yanawapa nguvu wakulima na wafugaji ya kujiona kuwa nao ni sehemu ya mafanikio ya serikali ya Tanzania.
Hata hivyo mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, licha ya kumpongeza mkulima huyo, amewashukuru wakulima, wafugaji na wadau wote wa halmasahuri hiyo, walioshiriki kwenye maonesho ya nanenane 2022, hata kama hawakuwa washindi wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya Kilimo na mifugo.
Aidha Mkurugenzi Msumi amewataka wakulima na wafugaji, kuwatumia Maafisa Ugani walio katika maeneo yao, kupata utaalmau sambamba na kujifunza teknolojia za kilimo cha kisasa ikiwa ni mkakati wa halmashauri kufikia Ajenda 10 - 30 ya Kilimo Biashara.
Kauli mbiu ya maonyesho ya Nanena 2022 ni Ajenda 10-30 Kilimo Biashara; Shiriki Sensa ya Watu na Makazi kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
PICHA ZA MATUKIO
Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere akimkabidhi kombe la Mshindi wa kwanza mkulima bora mkoa wa Arusha Isaya Lomayani, mara baada ya kufunga maonesho ya nanenane 2022 kanda ya Kaskazini, kwenye viwanja vya Themi -Njiro jijini Arusha.
Mkulima wa Kata ya Mwandet halmashauri ya Arusha, Isaya Lomayani akiwa ameshikilia kombe la ushindi wa Mkulima bora Mkoa wa Arusha mara baada ya kukabidhiwa na mgeni rasmi Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi akiwa ameshikilia kombe la ushindi wa Mkulima bora Mkoa wa Arusha Isaya Lomayan, mara baada ya kukabidhiwa na mgeni rasmi Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere.
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi akiwa kwenye picha ya pamoja na wakulima walioshiriki maonyesho ya nanenane kwenye banda la kilimo la halmashauri hiyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.