Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha ndugu Seleman Msumi, amempongeza na kumshukuru ndugu Bathlomeo Ngeseyan na rafiki zake kwa uzalendo wao wa kuchangia fedha kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni kumi kwaajili ya kutatua changamoto ya maji na ukaratabati wa majengo ya vyumba vya maabara katika shule ya Sekondari Losinoni iliyoko Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru.
“Mmefanya jambo la kizalendo sana na sisi kama serikali lazima tuwaunge mkono, kwasababu haya mliyoyafanya mmeweza kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa miundo na kuhakikisha wanafunzi wetu wanasoma bila tabu” alisema Msumi.
Sambamba na hayo, Msumi amewaonya wazazi wenye tabia ya kuwaozesha watoto katika umri mdogo na kwamba, Serikali iko macho na itachukua hatua kali kwa wale watakaothubutu kuua ndoto za watoto ambao kesho wanatarajiwa kuwa Viongozi wa Taifa hili.
Awali akisoma taarifa mbele ya Mkurugenzi, Mkuu wa Shule hiyo ndugu Emanuel Mkonongo ameeleza kuwa, akina Bathlomeo na rafiki zake wametekeleza mradi wa maji kwa kufanikisha ufungaji wa mifumo ya maji shuleni hapo kwa kutumia kiasi cha shilingi millioni 5,751,000/= ambapo zimetumika kujenga mnara wa kupandisha tenki la maji, kununua tenki la maji lenye ujazo wa lita elfu kumi, kujenga karo la wanafunzi kunawia mikono pamoja na kufunga mifumo ya maji kwenye vyoo vinne vya wanafunzi na walimu vyenye jumla ya matundu ishirini na mbili.
Vilevile wametumia shilingi million 5,200,000/= kuweka vioo vya madirisha na milango kwenye chumba kimoja cha maabara, kufunga mfumo na kuingiza umeme kwenye vyumba viwili vya maabara, kumalizia ujenzi wa choo cha walimu chenye matundu mawili, kununua TV na king’amuzi chake kwaajili ya walimu na wanafunzi.
Kwa upande wake ndugu Bathlomeo, Dkt. Paul Loisulie (PhD) na wenzake wamesema wameamua kufanya hivyo wakisukumwa na jitihada za serikali katika kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, vilevile Bathlomeo binafsi anatekeleza wosia wa marehemu baba yake ambapo wakati anafariki alimwambia somesheni watoto. Bathlomeo amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufaulu masomo yao sambamba na kulinda miundombinu hiyo kwaajili ya wengine.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.