Rais Mhe Dkt. John Pombe Magufuli azindua rasmi program ya ASDP II
Posted on: June 4th, 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli, amezindua rasmi programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa kimataifa la Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.
Akihutubia katika mkutano huo Rais Magufuli amezitaka sekta za kilimo, Sekta binafsi na Asasi za kiraia kujumuika pamoja katika kutelekeza mpango huo wa ASDP II ili kuongeza tija katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Viwanda.
Hata hivyo Mheshimiwa Rais ameiagiza wizara ya kilimo pamoja na wadau wengine wa kilimo kushughulikia kikamilifu changamoto zote zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa programu hiyo ya awamu ya Kwanza.
Aidha, ameongeza kuwa sekta ya kilimo ina nafasi kubwa ya kubadilisha hali ya uchumi wa nchi kuliko sekta za madini na gesi hivyo kilimo kiboreshwe ili kiweze kuleta mapinduzi katika sekta nyingine.Katika hatua nyingine Mhe. Rais ameitaka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) kusimamia malengo ya kuanzishwa kwake ili iweze kutoa msaada kwa wakulima ikiwemo kuwakopesha badala ya kufanya biashara baina ya benki na kuwakopesha wafanyakazi wake jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Awali waziri wa kilimo Mhe. Dkt.Charles Tizeba alisema kwamba Makadirio ya mahitaji ya rasilimali (Bajeti) kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo ni shilingi Trilioni 13 ambazo zitahitajika kutekeleza mpango huo kwa kipindi cha miaka 5 ya mwanzo.
“Mhe Rais Tayari kwa mwaka ujao wa fedha wa 2018/19, Serikali unayoiongoza inatarajia kuchangia kiasi cha Shilingi Bilioni 943 kupitia Wizara za Sekta ya Kilimo ambazo ni Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji” Alikaririwa Dkt Tizeba.
Aidha Halmashauri zote za Wilaya kupitia makusanyo yake ya ndani (Own sources) zinatarajia kuchangia kiasi cha Shilingi Bilioni 36”. Alisisitiza Dkt TizebaASDP II ni mpango wa miaka kumi utakaotekelezwa kwa awamu mbili za miaka mitano mitano kwa kuzingatia mazao yenye kuleta matokeo makubwa katika sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.Lengo la ASDP II ni kuendelea kuimarisha usalama wa chakula na Lishe nchini, kuongeza kipato cha wakulima na Taifa na pia kuchangia ukuajia wa sekta ya viwanda.
Mpango huu wa ASDP II utatekelezwa na wadau wote katika sekta ya Kilimo ambao ni Serikali, Sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo na Wakulima.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa, Wakuu wa mikoa mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dara es salaam Mhe Paul Makonda, Mawaziri wa sekta za kilimo viongozi vyama vya siasa, na dini na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.