Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela, amezindua mradi wa mashamba darasa matano ya ufugaji wa kuku kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali kwa vijiji vitano vya halmasahuri ya Arusha, mradi unaofadhiliwa na shirika la Hand in Hand East Africa Tz la mkoani Arusha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la kijiji cha Engora, Mhe. Mongela licha ya kulipongeza shirika kwa programu hiyo, amesisitiza shirika kufanya usimamizi na ufuatiliaji wa karibu kwa wanavikundi, ili mradi huo uweze kuimarika na kuwa endelevu na kuinua pato la kaya hizo.
Ameongeza kuwa, serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kupambana na umasikini nchini, na kusisitiza wanufaika hao, kusimamia mradi huo vizuri, ili kukuza mtaji kwa manufaa yao na kaya zao.
Aidha amelitaka shirika hilo kuongeza ukubwa wa mabanda na kuyaimarisha kuwa ya kisasa zaidi, ili kuongeza mitaji kulingana na idadi ya wanufaika kwenye vikundi, wanaotegemea miradi hiyo iweze kuwaongezea kipato na kuondokana na umasikini uliokithiri kama yalivyo malengo ya mradi.
"Kama lengo letu ni kuondoa umasikini, Hand in Hand tengenezeni mabanda makubwa na ya kisasa zaidi, ili yaweze kubeba kuku wengi zaidi, lakini pia vikundi viweze kukuza mitaji na kufanya miradi mikubwa, hapo ndio tunaweza kufikia lengo la kuondoa umaskini kama mlivyosema na niwaahidi nitafuatilia kuhakikisha mradi huu,unafanyika kwa kuzingatia vigezo mlivyoviainisha kwenye andiko lenu".Amefafanua Mhe. Mongela
Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, kuwapa kipaumbele wanavikundi hao pindi mikopo isiyo na riba itakapoanza kutolewa, ili waweze kuongezea mitaji yao.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Hand in Hand Jane Sabuni, amesema kuwa, kupitia mradi huo, shirika limejenga mashamba darasa matano ya ufugaji kuku kwa gharama ya shilingi milioni 51.5 na kuwapa mtaji wa vifaranga 200 kwa kila banda huku kila kikundi kikiongeza vifananga 100 na kufanya kila banda kuanza na mtaji wa vifaanga 300.
Ameyataja madhumuni ya mradi huo ni kupunguza umasikini kwa kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwajengea uwezo wa kuwa wajasiriamali kupitia vikundi vya wanawake, pamoja na kuwaunganisha na masoko ya bidhaa zitakazozalishwa.
"Ili kufanikisha ufugaji wenye tija, shirika limewapa mafunzo ya ufugaji wa kuku, utengenezaji wa chakula pamoja na vifaa vya kulishia 450 na kunyweshea 450, kwa wafugaji wakuku 380, kupitia vikundi vyao"Ameweka wazi Jane
Hata hivyo wanufaika wa mradi huo, wamelishukuru shirika hilo kwa msaada huo, na kuahidi kuusimamia vema kwa kuwa wanaamini unakwenda kuwaongezea pato na kuwanufaisha wao na kaya zao.
Stella Mollel amesema kuwa, licha ya mtaji wa waliowezeshwa na shirika la Hand in Hand, wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi na uendeahaji wa biashara, utunzaji wa fedha, kuweka na kukopa pamoja na kutengeneza chakula cha kuku hawa.
Awali, katika mashamba darasa hayo matano, jumla ya vifaranga 1000, vimetolewa kwa vikundi vya wanawake katika vijiji vya Likamba, Oltushula, Mirongoine na Engorora na kuhudumia wanachama 100 kwa kila kijiji.
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.