Na. Elinipa Lupembe.
Kufuatia uhusiano mzuri ya kirafiki, yaliyojengeka kati ya Tanzania na serikali ya watu wa Japani, Japani kupitia ubalozi wake nchini Tanzania, imeunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano, kwa kuchangia fedha kiasi cha shilingi milioni 191 na kukamilisha, ujenzi wa kituo cha kisasa cha Afya cha Manyire kata ya Mlangarini, halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru.
Ubalozi huo wa Japani umefikia hatua hiyo, baada kuridhishwa sera ya serikali ya kukabiliana na changamoto za huduma za afya, na kuamua kuwasaidia wananchi wa kata ya Mlangarini na vitongiji vyake, kuwaondolea na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya Kilomita 40 kwenda kupata huduma za afya kwenye hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho cha Afya, Balozi wa Japani nchini, Balozi Shininchi Goto, amesema kuwa, serikali ya Japani iligundua adha ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Mlangarini, ya kukosa huduma za afya katika maeneo yao, na kuamua kuwasaidia kumalizia ujenzi wa kituo chao cha afya, ambacho tayari walikuwa wameanza na kukwama kwa muda.
Balozi huyo amethibitisha kuwa, ukosefu wa huduma za afya karibu, ilikuwa ni hatari hasa kwa kina mama wajawazito na watoto, ambao baadhi yao walipoteza maisha kwa kuchelewa kupata matibabu, kulikosababishwa na umbali wa hospitali, huku akiamini kituo hicho cha afya kitaokoa maisha ya watu wengi tofauti na hapo awali.
"Serikali ya Japani imeamua kusaidia kuokoa maisha ya watu vinavyotokana na vifo visivyo vya lazima, vinavyotokana na kuchelewa kupata huduma, ninategemea mtakitunza kituo hiki ili kiweze kuwahudumia kwa muda mrefu" amesema Balozi Goto.
Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, licha ya kuishukuru serikali ya Japani, amesema kuwa msaada huo umetokana na mahusiano mema ya serikali na nchi ya Japani, yaliyojikita kwenye sera imara za serikali ya awamu ya tano ya kuboresha huduma za afya, kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msingi katika maeneo yao.
Ameongeza kuwa, uwepo wa kituo hicho cha Afya, utasaidia kutokomeza vifo vya wanawake na watoto, vilivyotokana na ukosefu wa huduma za haraka kwa wagonjwa na akifafanua kuwa, kwa sasa Kata ya Mlangarini imetekeleza adma ya serikali kwa asilimia 100, kwa kuwa na zahanati kwenye vijiji vyake vyote na kituo cha afya.
Hata hivyo, mwanzilishi wa ujenzi wa kituo hicho cha Afya, Diwani mstaafu wa kata ya Mlangarini, Mathias Manga ameshukuru serikali ya Japani, na amethibitisha kuwa na mkakati wa kutafuta fedha, kiasi cha shilingi milioni 150, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari na wauguzi, ili wananchi hao waweze kupata huduma kwa muda wote.
Naye Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, ameshukuru Ubalozi huo wa Japani na kufafanua kuwa, kituo hicho cha afya ni muhimu kwa wananchi wa eneo hilo na kinategemea kutoa huduma kwa zaidi ya watu 6,000 wa kata ya Mlangarini na vijiji vya kata jirani ya Bwawani, kata ambayo mpaka sasa haina kituo cha afya.
Ujenzi wa kituo hicho cha Afya, ulianza mwaka 2013 na kusimama kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa fedha, mwaka 2017 ndipo ubalozi wa Japani ulipoanza ujenzi na umekamilika kwa gharima ya shilingi milioni 468.6, huku shilingi milioni 120, Diwani Mathias Manga, milioni 20 nguvu za wananchi, milioni 83, serikali kupitia mapato ya ndani na ubalozi wa Japani milioni 191.
Balozi wa Japani nchini Tanzania, Balozi Shinichi Goto akikata utepe kuzindua kituo cha Afya Manyire kata ya Mlangarini.
Balozi wa Japani nchini Tanzania, Balozi Shinichi Goto akipiga makofi mara baada ya kukata utepe na kuzindua kituo cha Afya Manyire kata ya Mlangarini.
Balozi wa Japani nchini Tanzania, Balozi Shinichi Goto, akizungumza na mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro mara baada ya kuzinduliwa kwa kituo cha Afya Manyire kata ya Mlangari
Muonekano wa nyuma wa jengo la kituo cha Afya Manyire
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.