Na. Elinipa Lupembe
1Shirika lisilo la Kiserikali la HANDICAPPED CHILDREN REHABILITATION TANZANIA (HACRET) linajishughulisha na maendeleo ya watoto wenye mahitaji maalum Mkoani Arusha, limekabidhi vifaa vya kitaaluma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, shule ya Msingi Ilboru lengo likiwa ni kuwarahisishia watoto hao tendo la kujifunza na kufundishia.
Mkurugenzi wa Shirika la HACRET, Loy Yamat, wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha, amesema kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuwapatia wanafunzi wenye mahitaji maalum fursa ya kujifunza kwa uhuru zaidi na kuwasaidia kutimiza ndoto zao za kielimu.
“Tumekabidhi vifaa hivi kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 35 ili kuhakikisha watoto hawa wanakuwa na maaingira ya kujifunzia yakijumuisha na vifaa vya kisasa vya kujifunzia na ufunzaji”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Amevitaja vifaa alivyovikabidhiwa ni pamoja na makabati 10, viti na meza, vifaa vya stadi za Maisha na vifaa vya TEHAMA kompyuta mpakato 14, mashine ya kudurufu 1 na Projecta 1, vifaa ambavyo licha ya kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika shule hiyo, vitaongeza chachu ya wanafunzi kujifunza.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo na kuvikabidhi kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Ilboru kitengo maalum, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha Seleman Msumi, amelishukiru shirika hilo na kuwataka walimu pamoja na watumishi wote shuleni hapo, kuwasimamia wanafunzi kuvilinda na kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kutumika kama vilivyokusudiwa na hatimaye viweze kuwasaidia watoto hao kutimiza ndoto zao.
“Kikubwa ni shukrani sana kwa ndugu zetu wa HACRET, kama tunavyofahamu jamii yetu kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikiwaficha watoto wenye mahitaji maalum na ilikuwa inaonekana kama ni mkosi na aibu katika familia, lakini tumshukuru Mungu leo hii Serikali imefanya juhudi na kuhakikisha watoto hawa wanapata haki zao za msingi ikiwemo Elimu”. Amesema Mkurugenzi Msumi.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Philomena Mbilinyi amelishukuru shirika hilo kwa kuwaletea vifaa hivyo, ambavyo vinakwenda kutatua changamoto kubwa iliyokuwepo ya uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuahidi kuendelea kuvitunza na kuhakikisha vinatumika kwa matumizi fasaha ya kuwaletea wanafunzi hao mandeleo ya kitaaluma.
Hata hivyo wanafunzi hao wamethibitisha changamoto ya waliyokuwa wanakabiliana nayo hapo awali ikiwemo ya kukosa madaftari na kupelekea kuchapwa viboko na walimu ambapo sasa changamoto hiyo imepata mwarobaini.
“Madaftari tutapewa, hapo zamani tulikwa tunasumbuliwa na changamoto tulikuwa tukikosa madaftari na tukienda kuwamba walimu wanasema hawana na madarasani tunatandikwa fimbo, sasaivi tumepata ufadhili tutaendelea na masomo vizuri”. Amesema Mwanafunzi wa shule hiyo mwenye Ulemavu wa Ngozi, Feisal Mohemed.
Awali, hivi karibuni Serikali ilitoa fedha shilingi Milioni 50 kwaajili ya ujenzi wa uzio katika shule hiyo kwaajili ya kuhakikisha usalama wa wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu ambapo hadi sasa ujenzi huo umekamilika.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.