Na Elinipa Lupembe
Wadau wa maendeleo sekta ya elimu wa shirika lisilo la kiserikali la Kilimanjaro Education Foundation (KEF) wamejenga darasa maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu, kwenye kituo cha Elimu Maalum shule ya msingi Oldadai, halmashauri ya Arusha.
Shirika hilo limefikia uamuzi huo, mara baada ya kujionea, changamoto iliyokiwa inawakabili watoto wenye mahitaji maalum hususani walemavu wa viungo shuleni hapo, kwa kukosekana kwa miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi darasa hilo, Mkurugenzi wa shirika hilo, Bi. Michelle Land, amesema kuwa, baada ya kufadhili mradi wa maji shuleni hapo, waligundua changamoto wanayoipata watoto wenye ulemavu, shuleni hapo na kuamua kujenga jengo maalum lenye miundombinu rafiki, inayojumisha chumba cha darasa, vyoo maalum vya walemavu, mabafu, ofisi ya walimu, samani za ndani pamoja na viti mwendo mradi ulliogharimu kiasi cha shilingi milioni 48.
Michelle, ameweka wazi kufurahishwa na kitendo cha kukamilika kwa mradi huo, kwa kuwa anaamini malengo ya shirika ya kuwawezesha watoto wenye ulemavu, kusoma kwenye mazingira salama na rafiki yametimia na kuahidi kuendelea kutoa misaada mingine zaidi shuleni hapo.
"Leo nina furaha, kuona darasa hili limekamilika, ninaamini watoto hawa, watafurahia kusoma na kujifunza kwenye mazingira wezeshi kwao, kama wanavyofurahia kwa watoto wengine" Amesisitiza
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi amelishukuru shirika la KEF, kwa msaada huo wa thamani kwa watoto wenye mahitaji maalum, kwa kuwa utawawezesha watoto hao, kujifunza katika mazingira bora na salama zaidi hasa kwa afya zao.
"Tumepata darasa, kazi imebakia kwa wanafunzi kusoma kwa bidii, na walimu timizeni jukumu la kuwafundisha watoto hawa wa Mungu, hakikisheni darasa linaendelea kuwa safi kila siku, simamieni watoto kutunza miundombinu hii". Amesisitiza Mkurugenzi Msumi.
Naye Afisa Elimu Msingi, halmashauri ya Arusha, amesisitiza kuwa, uwepo wa mazingira rafiki kwa watoto wenye ulemavu shuleni, kunaongeza ari ya watoto hao kupenda shule pamoja na kujifunza zaidi, na kuwataka walimu kuhakikisha watoto hao, wanafikia ndoto na malengo yao.
Aidha amewataka walimu, pamoja na kutekeleza jukumu lao la kuwafundisha watoto hao, amewataka kuwasimamia wanafunzi kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Mkuu wa shule ya msingi Oldadai, mwalimu David David, licha ya kulishukuru shirika hilo, amesema kuwa hapo awali wanafunzi hao, walikabiliwa na changamoto ya miundombinu ya vyoo na chumba cha darasa, changamoto ambayo kwa sasa imemalizika katika kituo hicho.
Aidha amewata wazazi wenye watoto wenye ulemavu, kuwapeleka watoto hao shule kwa kuwa wanafundishika kama ilivyo watoto wengine na kuwaonya baadhi ya wazazi kuacha kuwaficha watoto hao kwa kuwa serikali imeweka mazingira rafiki ya kujifunzia maalum kwa watoto hao.
Awali Kitengo cha Elimu Maalum shule ya Msingi Oldadai, kina jumla ya wanafunzi 35 wavulana 19 na wasichana 16 wote wakiwa ni walemavu wa viungo.
SHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI
JIANDAE KUHESABIWA✍✍✍
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA MAKABIDHIANO YA MRADI WA JENGO LA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU SHULE YA MSINGI OLDADAI.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi na Mkurugenzi wa Shirika la Kilimanjaro Education Foundation, Michelle Land wakikata utepe kama ishara ya kufungua jengo la wanafunzi wenye ulemavu shule ya Msingi Oldadai.
Jengo Maalum la Wanafunzi wenye Ulemavu shule ya Msingi Oldadai, lililojengwa na shirika la Kilimanjaro Education Foundation kwa gharama ya shilingi milioni 48.
Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi akimkabidhi cheti cha shukurani, Mkurugenzi wa Shirika la Kilimanjaro Education Foundation Michelle Land, mara baada ya kukabidhiwa jengo la wanafunzi wenye ulemavu shule ya Msingi Oldadai.
Mkurugenzi wa Shirika la Kilimanjaro Education Foundation, Machelle Land, akihutubia wananchi wa Oldadai wakati wa hafla ya makabidhiano ya jengo la wanafunzi wenye ulemavu shule ya Msingi Oldadai.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.