Na. Elinipa Lupembe.
Shirika lisilo la kiserikali la World Serve International Tanzania, lenye makao yake makuu Jijini Arusha, mradi wa maji kwa halmashauri ya Arusha, mara baada ya kuzindua mradi huo, mradi uliojengwa kwa ufadhili wa shirika la 'Water Boys' la nchini Marekani kwa gharama ya shilingi milioni 200.
Akizungumza wakati wa kumkabidhi mradi huo, kwenye hafla fupi iliyofanyika katika shule ya msingi Sekei, Mratibu wa Mradi, shirika la World Serve International Tanzania, Elyne Kingu amesema kuwa, lengo kuu la mradi huo ni kuhudumia wanafunzi wa shule za Naurei, Sekei na shule mpya ya sekondari Kiutu, baada ya kupokea ombi kutoka kwa uongozi wa kijiji cha Naurei.
Kingu ameongeza kuwa, kwa kipindi kifupi cha kukamilika kwa mradi huo, tayari matokeo yameanza kuonekana, kutokana na mabadiliko ya usafi wa mazingira unaonekana wazi na unaoashiria, uhakika wa afya za wanafunzi hasa watoto wa kike kuweza kujistiri wakati wa siku zao za hedhi.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, licha ya kulishukuru shirika hilo, ameahidi kuusimamia mradi huo, uweze kujiendesha na kuwa endelevu pamoja na kuhudumia jamii inaozunguka eneo hilo la shule.
Amesisitiza kusimamia mradi huo vizuri na kuongeza idadi ya watu kupata maji hayo, kutokana na ujazo wa maji, yanayotokana na chanzo hicho,kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 20,000 kwa saa, ujazo ambao ukisimamiwa vizuri, unauwezo wa kuhudumia idadi kubwa zaidi ya watu waliokusudiwa.
Hata hivyo amefafanua kuwa, kazi iliyofanywa na shirika hilo ya kutukuka, ni ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha ifikapo mwaka 2020, asilimia 80 ya watu vijijini wanapata maji safi na salama, pamoja na utekelezaji wa uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati, ifikapo 2025.
Naye, Mkurugenzi wa Maji shirika la 'Water Boys' la nchini Marekeni, Nicole Woods, amesema amefurahishwa kuona wanafunzi wanafurahia huduma ya maji, na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali kufanyakazi na shirika hilo, na kusisitiza mradi huo kutumika kwa lengo lililokusudiwa la kuwapa huduma ya maji safi na salama wananchi, pamoja na kuweka mipango imara ya usimamizi wa mradi huo, ili uwe endelevu kwa miaka mingi ijayo.
"Nilipokuja kwa mara ya kwanza hapa shuleni, hakukuwa na maji, watoto waliteseka, leo nimefurahi kukuta maji yanatoka na wanafunzi wanafurahia huduma hiyo, ninaishukuru Serikali ya kukubali kufanyakazi na sisi, jambo la muhimu ni mradi huu kutunzwa na kutumika kwa miaka mingi ijayo" amesema Nicole
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sekei, mwalimu Adam Sambo, amethibitisha kuwa, kwa sasa hali ya usafi wa mazingira ya shule, imebadilika sana, tofauti na hapo awali, wanafunzi wana furaha kutokana na kuwa na uhakika na afya zao, wameotesha vitalu vya maua na mbogamboga, mboga ambazo zinatumika kwa ajili ya chakula chao, pamoja na kujifunza elimu ya kujitegemea.
"Awali tulipata shida sana ya kupata maji katika eneo letu la shule, tulishindwa kupata maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi shuleni, maji ya kunywa, ya kupikia na hata ya kunawa mikono mara baada ya kutoka chooni, hali ya watoto wa kike kujisiri wakati wa hedhi ilikua ni shida, lakini sasa huduma hii ya maji imeboresha na kuhakikisha usalama wa wanafunzi na walimu wawapo shuleni" amefafanua mwalimu Sambo.
Awali fedha hizo za mradi zimetumika katika shughuli za uchimbaji wa visima vitatu na mpaka sasa visima viwili ndio vilifanikiwa kupata maji, tanki la lita elfu 60, pumpu zinazotumia umeme wa jua, pamoja na vituo 8 vya kuchota maji.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.