Halmashauri ya Arusha, imepokea msaada wa vifaa vya kufanyia usafi, vyenye thamani ya shilingi milioni 2, msaada uliotolewa na Kiwanda cha kutengeneza nyuzi na nguo, SUNFLAG cha Jijini Arusha.
Akizungumza kwa njia ya simu, meneja wa Kiwanda cha Sunflag, Harun Mahundi, amesema kuwa, lengo la kutoa vifaa hivyo, ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano, inayosisitiza suala la kufanya usafi wa mazingira, pamoja na kudumisha uhusiano mzuri baina ya kiwanda hicho na halmashauri ya Arusha.
Ameongeza kuwa, ni kawaida ya kiwanda kutumia asilimia kidogo ya faida wanayopata, kurudisha fadhila kwa wateja wake, ambao ndio wananchi, na kuvitaja vifaa hivyo ni pamoja na matoroli, mifagio, mafyekeo, majembe, reki, mikasi, buti, makoti, na vifaa vya kukusanyia taka.
Naye mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, ameushukuru uongozi wa kiwanda hicho, na kusema kuwa, serikali inathamini michango ya wadau wa maendeleo, ndio sababu imeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji kwa faida ya wananchi hasa watanzania wa hali ya chini kiuchumi.
"Nishukuru kiwanda cha Sunflag kwa msaada huu, unaokwenda kusafisha magulio, ambayo kwa kiasi kikubwa yanawahudumia wananchi wetu, wasio na uwezo mkubwa kiuchumi" amesema Dkt. Mahera.
Aidha Afisa Usafishaji na Mazingira, halmashauri ya Arusha, Marlaw Msuya, amesema kuwa, vifaa hivyo vimekuja wakati muafaka, kutokana na changamoto ya uhaba wa vifaa vya kufanyia usafi iliyokuwepo, inayosababishwa na ukubwa maeneo yanayofanyiwa usafi na halmashauri yenyewe kwa sasa.
Nao wafanyakazi wa Idara ya Usafishaji, wamekiri uwepo wa vifaa hivyo utaongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya ukufanya usafi, huku vikiwahakikishia usalama wa afya zao pia.
Abdala Maigisa, amesema kuwa, wanafanya usafi na kukusanya taka kwenye maeneo ya masoko ambapo kuna taka za kila aina, hivyo kutokuwa na vifaa kama glovusi, buti na vizolea taka, mara nyingi huhatarisha usalama wa afya zao na kufanyakazi kwa hofu, lakiji uwepo wa vitendea kazi imara, utaongeza kasi na ari ya kazi.
" Tunasafisha na kukusanya mchanganyiko wa kila aina ya taka, hivyo bila vifaa ni hatari kwa afya zetu, unaweza kuchomwa na taka zenye ncha, unaweza kupata hata maradhi ya kuambukizwa, vifaa hivi vitasaidia kufanyakazi zetu bila hofu" amesema Maigisa.
Halmashauri ya Arusha, kupitia Idara ya Usafishaji na Mazingira, imekuwa mstari wa mbele kutekeleza agizo la makamu wa Rais mama Samia Suluhu la kufanya usafi kila mwisho wa mwezi na kuhakikisha mazingira yote yanakuwa safi kwa afya ya wananchi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.